NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa viti maalum kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Zuena Bushiri amewataka vijana wa Chama cha Mapinduzi kujenga mahusiano mazuri na wananchi pamoja na kuwahamasisha kuwachagua viongozi wanaotokana na chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 27 mwaka huu.
Bushiri ametoa kauli hiyo leo alipokutana na vijana wa chama hicho katika ofisi za CCM wilaya ya Moshi vijijini ambapo alisema kuwa vijana ni jeuri ya chama na kinawategemea katika ushindi wa Novemba 27 mwaka huu.
Alisema kuwa, chama hicho kimefanya mambo makubwa kwa wananchi na kuwataka kuwa mstari wa mbele kuyasemea yale yote mazuri yaliyofanywa na chama hicho ili wananchi waweze kutambua na kuelewa ni kwanini wawachague wagombea wa CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Katika hatua nyingine Mbunge huyo amefanya kikao cha ndani na wanachama wa CCM kata ya Kimochi na pia kukutana na Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM kata ya Old Moshi Magharibi Jimbo la Moshi vijijini lengo likiwa ni kuwahamasisha kwenda kuomba kura kwa wananchi.
Alisema kuwa, wananchi wanawajibu wa kuwachagua viongozi bora watakaokwenda kuwaletea maendeleo katika kipindi cha miaka mitano ambapo viongozo hao wanatoka ndani ya CCM.
"Wapo watu ambao wamekuwa wakipita pita na kuwadanganya wananchi ili wawachague wakati wao wenyewe hawana hata ofisi za kata hata wilaya mtakapowachagua watu hao mtakuja kuwaonea wapi..? Ni wajibu wetu sisi Wanaccm kuwaelimisha wananchi wasije kudanganywa" Alisema Mbunge Zuena.
0 Comments