NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameungana na viongozi mbalimbali wa CCM Taifa, Mkoa, Wilaya na Kata kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa katika maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro.
Akiongoza uzinduzi wa kampeni hizo katika eneo la Boma Mbuzi, mlezi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Rabia Abdalla Hamid ambaye ni Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Siasa na Uhusiano wa Kimataifa aliwasihi wananchi wa mkoa huo kuwachagua wagombea wa Chama Cha Mapinduzi katika ngazi mbalimbali.
Alisema kuwa, serikali ya CCM inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imewatendea haki wana Kilimanjaro kwa kuwaletea miradi mingi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 900 kama ilivyothibitishwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Patrick Boisafi.
Alisema, CCM ni chama kikongwe barani Afrika kinachojali wananchi wake na kuwaambia wana Kilimanjaro kuwa fursa za maendeleo zinapatikana CCM na si kule kwenye vyama vingine.
Alitoa mifano mingi ya mambo makubwa yaliyofanywa na serikali ya CCM ikiwemo miradi ya reli ya umeme (SGR), mradi wa umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa miundombinu ya barabara na maji, na usambazaji wa nishati ya kupikia kwa akina mama nchini.
Mbunge Ndakidemi alipata fursa ya kushiriki katika uzinduzi wa kampeni katika kijiji cha Boro ambapo amezaliwa.
Akiongea na mamia ya wanakijiji wa Boro, Ndakidemi aliwaomba wanakijiji wenzake wakipe Chama cha Mapinduzi kura za heshima kwa kumchagua, Laurent Mushi na timu yake kwani katika awamu ya uongozi iliyopita alisimamia kikamilifu miradi mbalimbali ya maendeleo hapo kijijini ikiwemo ile ya kuipandisha hadhi Shule ya Sekondari Masoka.
Miradi mingine ni uboreshaji wa barabara ya Boro Sangiti, ujenzi wa ofisi mpya ya Kijiji cha Boro, ukarabati wa eneo korofi la kwa Shah, ujenzi wa daraja la Kitara kyamburu na ile ya upatikanaji maji na umeme wa uhakika katika Kijiji cha Boro.
Alisema, Mushi alisimama imara kulinda raslimali za kijiji na usalama na amani kwa wanakijiji wake.
Akizungumza katika Kijiji cha Sambarai kilichoko katika Kata ya Kindi, Ndakidemi aliwaomba jirani zake hao wamchague Shio na timu yake.
Aliwaambia wananchi kuwa ushindi kwa CCM katika uchaguzi huo utakuwa na tija na manufaa makubwa kwa wananchi wote wa Sambarai kwani kwa kushirikiana na Diwani na Mbunge, watatatua kero zao kwa vitendo.
Mwisho..
0 Comments