Header Ads Widget

BINTI WA MIAKA 9 ADAIWA KULAWITIWA UHAMBINGETO IRINGA ,JAMII YAHOFU ...

 

Na Zuhura Zukheri,Matukio Daima media Iringa

INASIKITISHA tukio la Binti wa Miaka 9 mkazi wa kijiji cha Uhambingeto, Kata ya Uhambingeto, Wilaya ya Kilolo, Mkoa wa Iringa,anayepewa jina la Rose (sio jina halisi), anadaiwa kulawitiwa na kijana anayejulikana kama Stephano Chengula, mwenye umri wa miaka 18. 

Tukio hili linaripotiwa kutokea mnamo Novemba 2, saa sita mchana, wakati Rose alipokuwa akitoka kuchota maji kwenye bomba la kijiji, ambapo mtuhumiwa alimtokea na kumvuta hadi ndani kwao, akimfanyia ukatili huo licha ya kelele alizopiga.


Bibi wa binti huyo, Anita Lyegu, alieleza kuwa alihisi wasiwasi baada ya kumtuma mjukuu wake kuchota maji na kuona muda mrefu umepita bila kurudi.

 Alipokuwa anamtafuta na kumuita, ndipo alipoona kijana huyo anatoka ndani huku binti huyo akiwa analia na kueleza kilichotokea. 

Mtoto huyo alikimbizwa katika zahanati ya kijiji ambapo ilithibitishwa kuwa amelawitiwa, na familia hiyo ilichukua hatua ya kisheria kwa kumfikisha mtuhumiwa polisi.



Shangazi wa binti huyo, Riziki Mnyagala, ameitaka serikali kuhakikisha haki inatendeka kwa mtuhumiwa, akisema kuwa hawako tayari kumaliza suala hili kienyeji kama inavyofanyika mara kwa mara katika kijiji hicho.

 Mnyagala aliongeza kuwa tukio hilo limemwathiri kisaikolojia binti huyo, ambaye ni yatima na hivi karibuni amepoteza mama yake.

Mtendaji wa Kijiji cha Uhambingeto, Issa Ngaga, alithibitisha kupokea taarifa hiyo na kusema kuwa suala hilo limefikishwa mikononi mwa sheria, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kutojaribu kumaliza masuala haya kwa kulipana fidia, kwani huendelea kuathiri watoto kisaikolojia.

Watoto wanaokumbwa na ukatili wa kijinsia kama ulawiti na ubakaji hukumbana na madhara makubwa, ambayo yanaweza kuwa ya muda mrefu:

Ifahamike kuwa Madhara ya Kisaikolojia: Watoto wanaokumbwa na ukatili wa kijinsia mara nyingi hupatwa na msongo wa mawazo, hofu, na sonona. 

Pia hukosa kujiamini na wakati mwingine hujitenga na jamii kwa hofu ya kudhalilika au kunyanyapaliwa. Ukatili kama huu unaathiri sana afya ya akili na kuathiri mahusiano ya mtoto na watu wengine.


Pia  Watoto wanaoweza kuathirika kimwili na kupata majeraha yasiyopona au maambukizi ya magonjwa ya zinaa ambayo yanaweza kuwa hatari kwa afya yao ya baadaye.


Madhara mengine ya kisaikolojia na kimwili yanaweza kuathiri utendaji wa mtoto shuleni na uwezo wake wa kimaendeleo. Watoto waliopitia ukatili wanapoteza hamu ya kujifunza na mara nyingi wanashindwa kufikia malengo yao kimasomo na kimaisha.

 Ukatili wa kijinsia unaweza kuathiri mtazamo wa mtoto kuhusu mazingira yake, hali inayosababisha hofu, wasiwasi, na msongo wa mawazo ambao unaweza kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya kisaikolojia na kimwili.

Ili kuzuia madhara haya, jamii inapaswa kushirikiana na mamlaka husika katika kupinga vikali vitendo vya ukatili na kuhakikisha haki inatendeka badala ya kumaliza masuala haya kienyeji.

 Kuelimisha jamii kuhusu madhara haya pia ni muhimu ili watoto waweze kukua katika mazingira salama na yenye afya.

TAZAMA FULL VIDEO YA TUKIO LA KULAWITIWA BOFYA LINK HII

WASILIANA NA MATUKIO DAIMA MEDIA PIGA SIMU 0754026299

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI