Na Fatma Ally, Matukio DaimaApp, Dar
Wanawake Nchini Tanzania hususani wasichana wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi hususani katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka huu na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani ili kuwa Sehemu ya kufanya maamuzi katika masuala mbalimbali ya Jamii na Taifa.
Wito huo umetolewa Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Watoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mathias Haule wakati akizungumza katika kuelekea kilele cha kampeni ya kuhamasisha watoto wa Kike kushika hatamu za Uongozi iliyoandaliwa na Shirika la Kimataifa la Plan kwa lengo la kuwajengea Uwezo.
Amesema kuwa, wanahamasisha watoto kuhamasisha wazazi wao kushiriki katika uchaguzi wa serikali za Mitaa mwaka huu na uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani mwezi October, kwani watoto wa kike wana nafasi kubwa ya uongozi na uongozi lazima ujifunze ambapo kujifunza lazima itokane na watu wenye uzoefu.
Amesema kuwa, kampeni ya Girlstakeover imeenda sambamba na kauli mbiu ya siku ya mtoto wa kike kimataifa inayosema "Mtoto wa kike na uongozi,tumshirikishe wakati ni Sasa" ,hivyo serikali kwa kushirikiana na Plan International itahakikisha watoto wa kike wanapata nafasi za uongozi katika maeneo mbalimbali hasa wakiwa mashuleni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika hilo la Plan nchini Tanzania Jane Sembuche amesema watoto zaidi ya 40 wamefanyakazi kama viongozi katika Taasisi na Balozi mbalimbali na hivyo kujengewa uwezo wa kutosha na kwamba wanaamini wengi wao watatimiza ndoto za kuwa viongozi huku akisema jitihada za kumsaidia Mtoto wa kike zimekuwa na mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali.
"Siku yetu ya leo ambayo tunaiita Girls takeover au wasichana kushika hatamu ni kampeni ambayo Plan International kwa Tanzania na Nchi mbalimbali Duniani ambapo Plan ipo hua tunafanya kila mwaka ikiwa ni sambamba na kusherehekea siku ya watoto wa kike duniani ambayo hufanyika Oktoba 11 Kila Mwaka" amesema.
Aidha amesema kuwa wasichana wanaweza kuwa viongozi wazuri katika jamii, nakwamba kitu cha msingi ni kuweka juhudi , malengo na kujiamini yeye kama msichana anaweza kufikia malengo yake na anaweza kua kiongozi katika jamii na kuleta mabadiliko yanayotakiwa.
Akizungumzia suala la uchaguzi wa Serikali za mitaa amesema kuwa pamoja na shirika hilo kutekeleza Kampeni ya Girls takeover lakini pia lina kampeni nyingine ya "Sikia Sauti zetu "ili kuwezesha sauti za wasichana sehemu mbalimbali wanahamasika kuzungumza nakuleta changamoto zao katika sehemu husika.
"Tunaamini wanaendelea kukuzika katika uongozi kuanzia ngazi za jamii na kupata uzoefu kwahiyo nikuhamasisha wote ambao wana uwezo wasifikirie kama kitu kigumu,wajitokeze kuwania nafasi hizo" amesisitiza.
Nao baadhi ya Wasichana kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es salaam walioshiriki katika Kampeni hiyo pamoja na Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari kutoka Mkoa wa Katavi wamesema wamejifunza mambo mengi katika Kampeni ikiwa ni pamoja na kutumia muda vizuri huku wakitoa wito kwa Wasichana wanatamani kuwa Viongozi kuongeza bidii na kutokata tamaa.
Kampeni hiyo ni sehemu ya kuelekea Maadhimisho ya Mtoto wa Kike Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba 11.
0 Comments