Header Ads Widget

WANANCHI WAGUSWA MIAKA 60 YA HIFADHI YA RUAHA

NA HERIET MOLLA MATUKIO DAIMA MEDIA 

KATIKA kuadhimisha miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyoko mkoani Iringa, wafanyakazi wa Hifadhi hiyo  wamekuwa Nuru kwa jamii baada ya kutoa  misaada mbalimbali kama shukrani kwa ujirani mwema na mchango wao katika uhifadhi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa sherehe hizo, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Godwell Ole Meingataki, alisema misaada hiyo ilitolewa kwa vijiji vinavyopakana na hifadhi, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea mafanikio ya hifadhi hiyo pamoja na kudumisha mahusiano mazuri na wananchi.

Ole Meingataki alieleza kuwa misaada hiyo iligawiwa kwa wananchi wa vijiji vitano vinavyopakana na hifadhi, ambavyo ni Idodi, Tungamalenga, Mapogoro, Kisirwa na Mahuninga. Misaada hiyo iliwalenga hasa wananchi kutoka kwenye mazingira magumu, ikiwemo watu wanne wenye ulemavu waliopatiwa viti vya magurudumu. Aidha, zaidi ya wanafunzi 40 walinufaika kwa kupata sare za shule, viatu, na mabedi yenye mfumo wa sola ili kuwawezesha kusoma nyakati za usiku. Vilevile, wananchi walipewa msaada wa unga wa kilo 50, lita 10 za mafuta ya kupikia, na boksi moja la sabuni kwa kila mmoja.


Katika hotuba yake, Ole Meingataki alisisitiza kuwa mafanikio haya yametokana na ujirani mwema kati ya hifadhi na jamii zinazozunguka hifadhi hiyo, huku akiahidi kuwa kutakuwa na miradi mikubwa zaidi ya kusaidia jamii.

Kamanda wa Uhifadhi wa Kanda ya Kusini wa TANAPA, Naibu Kamishna Steria Ndaga, aliyemwakilisha Kamishna wa TANAPA, alisisitiza kuwa maadhimisho haya ya miaka 60 ni fursa ya kuweka malengo ya kuendelea kuhifadhi hifadhi ya Ruaha kwa ajili ya vizazi vijavyo. Alipongeza pia mchango mkubwa wa jamii zinazozunguka hifadhi hiyo katika mafanikio hayo.

Kheri James, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, aliyekuwa mgeni rasmi, alibainisha kuwa maadhimisho haya yanatoa nafasi kwa hifadhi na wakazi wa maeneo ya jirani kusherehekea mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mingi na kutafakari changamoto zilizopo. Alieleza kuwa ndani ya miaka 30 iliyopita, miradi 93 imekamilishwa kwa ajili ya wananchi, yote ikiwa imefadhiliwa na Hifadhi ya Ruaha. Alisisitiza kuwa ushirikiano wa ujirani mwema unapaswa kuendelezwa kwani uwepo wa hifadhi hiyo ni fursa muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa pongezi kwa TANAPA na uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa kufanikisha hafla hiyo iliyoleta watu wa aina mbalimbali pamoja, hasa kutoka maeneo jirani.

Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Tanzania, Shigeki Komatsubara, alitoa pongezi zake kwa TANAPA na Hifadhi ya Ruaha kwa jitihada zao za kuendelea kuboresha mazingira ya hifadhi hiyo. Aliahidi ushirikiano zaidi kati ya UNDP na Tanzania katika masuala ya uhifadhi.

Emakulata Changwa na Thomas Kiwele, miongoni mwa walemavu wanne waliopatiwa viti vya magurudumu, waliushukuru uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa kuwajali na kutambua mahitaji yao.

Diwani wa Kata ya Idodi, Julius Mbuta, ambapo maadhimisho hayo yalifanyika, alielezea namna Hifadhi ya Ruaha imechangia katika maendeleo ya wananchi kwa kufadhili miradi ya shule na zahanati, hatua ambayo imesaidia kupunguza gharama kwa wananchi waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Wananchi waliohudhuria walitoa ushuhuda wa namna elimu ya ujirani mwema imewasaidia kuelewa umuhimu wa kulinda rasilimali zao, hasa wanyamapori, na jinsi ambavyo wamekuwa wakitoa elimu ya kupinga ujangili kwa wenzao.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI