Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),Mkoa wa Morogoro,wakiwapatia huduma ya ulipaji wa kodi baadhi ya Wafanyabiashara katika Manispaa ya Morogoro,baada ya kuweka kambi katika eneo la Soko Kuu la Chifu Kingalu lilopo Manispaa ya Morogoro, picha na Ashton Balaigwa.
Na Ashton Balaigwa,MOROGORO
WAFANYABIASHARA Mkoani Morogoro wameonyeshwa kuridhishwa na hatua ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),kwa kuweka kambi katika maeneo mbalimbali ili kuwapatia huduma za ulipaji kodi kwa wakati na kuwaepusha kulipa faini baada ya muda wa ulipaji uliwekwa kufikia tamati.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa utoaji wa huduma za mlipakodi katika Soko Kuu la Chifu Kingalu , Manispaa ya Morogoro , wafanyabishara hao walisema,kuwekwa kwa kambi hizo inachangia huduma kuharakisha kwao ulipaji kodi kwa wakati na kuepukana na kutozwa riba .
Mfanyabiashara Shabani Kibuhile alisema kwa sasa Mamlaka hiyo imekuwa na desturi ya kutoa huduma rafiki kwa jamii tofauti na miaka iliyopita ambapo njia waliyokuwa wakiitumia iliwafanya wafanyabishara kuwakimbia na kuwaona ni maadui.
Kibuhile alisema kuwa , wananchi wakiwemo wafanyabiashara wanapolipa kodi kwa wakati wanachangia upatikanaji wa huduma bora kwa Watanzania zikiwemo za miundombinu ya barabara ,huduma za afya ,elimu na nyingine mtambuka.
“ Hivi sasa TRA huduma zao zimekuwa rafiki kwa sisi wafanyabiashara kwani wanatoa elimu, kushauri, kuelekeza masuala ya msingi na umuhimu wa kulipa kodi yenyewe ndiyo maana wamekuwa wakitufuata tulipo tofauti na miaka ya nyuma ilikuwa ni kukimbizana “alisema Kibuhile.
Mfanyabiashara huyo aliwashauri wananachi na wenzake kujenga utaratibu wa kufuata sheria ulipaji kodi wakitambua Mamlaka hiyo ina jukumu la kusimamia sheria za kodi ili kuiendeleza nchi yetu ,na nchi haiwezi kuendelea bila kulipa kodi .
Naye mfanyabiashara , Ijumbo Majani ,alisema kusongezwa kwa huduma za Mamlaka hiyo karibu yao imewarahisishia kuipata huduma za mlipakodi bila ya kukabiliana na changamoto ikiwa ya kuwafuata ofisini kwao.
“ Nimekuja hapa kwenye kituo cha Soko Kuu la Chifu Kingalu na nimetumia dakika chache kuhudumiwa huduma ya malipo serikalini na ninarudi kuendelea na biashara zangu “ alisema Majani.
Majani alishauri huduma iwe ni endelevu kwa kuwa itawawezesha wananchi na wafanyabiashara kulipa kodi kwa muda unaopangwa licha ya wao kutambua ni wajibu wao kulipa kodi ya serikali.
Kwa upande wake Ofisa Huduma na Elimu ya Mlipakodi wa TRA mkoa wa Morogoro, Immaculate Chaggu alisema, huo ni mwendelezo wa kukusanya mapato kwa kutoa namba ya malipo ya serikali kwa wafanyabiashara na utoaji elimu ya mlipa kodi.
“ Tumeweka Kambi katika maeneo matatu ikiwemo eneo la Soko Kuu la Chifu Kingalu ili tuwahamasishe walipa kodi waweze kulipa kodi yao kwa awamu ya tatu bila shuruti ili wasiweze kupata riba baada ya muda kupita “ alisema Chaggu .
Alisema huduma zimesongezwa karibu na wananchi kwa kuweka vituo vitatu ambavyo ni Soko Kuu la Chifu Kingalu , Kihonda na Mkundi katika Manispaa ya Morogoro.
Chaggu alisema vituo hivyo vilianza kutoa huduma Septemba 21, mwaka huu na zaidi ya wateja 100 wanahudumiwa kwa siku na kadri zinavyo karibia mwisho wa kufikia Septemba 30, mwaka huu idadi inaendelea kuongezeka kwa siku.
Ofisa Mwandamizi wa Kodi wa Mamlaka hiyo mkoani Morogoro, George Mkope ,alisema kupitia utekelezaji wa huduma hiyo kumekuwa na mwamko mkubwa wa wananchi kulipa kodi kwa hiari na njia hiyo imeongeza morali kwao kujitokeza kulipa kodi kwa hiari .
“ Tunakusudia kuongea vituo zaidi ili tuwafikie watu wengi walipe kodi kwa wakati na tufikie yale malengo tuliyopewa na serikali ya kukusanya kodi “ alisema Mkope.
0 Comments