Matukio daima Rukwa Elizabeth Ntambala
Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limezindua rasmi kampeni ya "Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa" katika wilaya ya Nkasi. Kampeni hii inalenga kuwalinda vijana dhidi ya changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri fikra na tabia zao. Uzinduzi huo, uliowakutanisha wadau kutoka sekta mbalimbali, ulifanyika katika hafla iliyohudhuriwa na watu takribani 700.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mheshimiwa Peter A. Lijualikali, ambaye amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia Kamisheni ya Polisi Jamii na Dawati la Jinsia na Watoto.
Kampeni hii ilizinduliwa kitaifa tarehe 29 Agosti 2024 mkoani Njombe. Lengo kuu la kampeni ni kuwasaidia wanafunzi wa vidato vya kwanza, vidato vya tano, vyuo vya kati, na vyuo vikuu kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazowakumba wanapoanza masomo yao. Kampeni inalenga kuwajenga kiakili na kitabia ili waweze kuepuka athari mbaya za mazingira wanayokutana nayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Shadrack Masija, amewataka maafisa na wadau kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa jamii, hasa vijana. Alisisitiza kuwa kampeni hiyo inalenga kuwa msingi wa kuzuia vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika jamii za Tanzania.
Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Rukwa, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ACP) Faustina Mwakapangala, amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika Hafla hiyo inadhihirisha ishara ya kuungwa mkono kwa kampeni hii muhimu.
Aidha, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Nkasi, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Atupele Mwakaliku, pamoja na Afisa wa Polisi Jamii Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Zacharia Bura, walitoa shukrani zao kwa wadau wote waliojitokeza katika hafla ya uzinduzi huo.
Kampeni ya "Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa" inatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii kwa kuwajengea wanafunzi na vijana ujasiri wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili.
0 Comments