Na Fadhili Abdallah, Kigoma
Wadau wa haki jinai mkoa Kigoma wamefanya ziara kutembelea shughuli za mamlaka ya bandari katika bandari ya Kigoma na Kibirizi mjini Kigoma ili kuwezesha kuwa na uelewa mpana wa shughuli za bandari iweze kuwasaidia yanapotokea mashauri mahakamani kuhusiana na jambo lolote la kesi za jinai na madai zinazotokea bandarini.
Mkurugenzi wa huduma za sheria wa Mamlaka ya bandari nchini (TPA), Stanslaus Kagisa akizungumza wakati wa warsha ya siku mbili kwa wajumbe wa kamati ya Haki jinai mkoa Kigoma alisema kuwa TPA imelifanya jambo hilo kuwapa uelewa na kujua kwa undani shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo ili shughuli za mashauri ya kisheria zinazohusu mamlaka hiyo ziweze kushughulikiwa kwa haraka na kwa uelewa mpana.
Kagisa alisema kuwa serikali inafanya uwekezaji mkubwa katika bandari zake ikiwemo bandari za ziwa Tanganyika ikiwemo za mkoa Kigoma hivyo mabilioni hayo yanaongeza hatari yakuongezeka kwa mashauri ya jinai hivyo Majaji,Mahakimu, wapelelezi, ofisi ya Mwendesha mashitaka wanapojua kwa undani shughuli za bandari watasaidia kuharakisha kesi lakini maamuzi yao kuzingatia sheria na hasara inayoweza kupatakana katika uwekezaji huo.
Alisema kuwa ziara waliyofanya katika bandari za mkoa Kigoma inawapa picha ya namna gani wasimamie kesi hizo kwa uharaka wake na kwa maslahi ya Taifa hasa kwa miradi ya kimkakati kama hii ya bandari hivyo ziara hiyo kwao imekuwa na manufaa makubwa katika kurahisisha utendaji kazi wao.
Kwa upande wake Mkuu wa Upelelezi na makosa ya jinai mkoa Kigoma, Alfred Kasolo alisema kuwa bandari ni eneo la kiuchumi na biashara ambalo linatoa fursa ya upatikanaji wa pesa hivyo kuwepo kwa makosa mengi ya jinai na madai hivyo wao kama wadau wa haki jinai mafunzo na ziara hiyo itakuwa na tija kubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya upelelezi.
0 Comments