Na Fadhili Abdallah, Kigoma.
Viongozi wa vyama vya siasa mkoani Kigoma wamepongeza hatua ya serikali mkoani humo kuwashirikisha viongozi wa vyama vya siasa katika uhamasishaji wa zoezi la uandikishaji wapiga kura kwenye daftari la mkazi kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa serikali na kufanikisha zoezi kwa kiasi kikubwa.
Viongozi hao walitoa pongezi hizo kwa Mkuu wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye kwa kuwezesha viongozi hao kutembea mkoa Mzima kufanya uhamasishaji huo ambapo gharama ya zoezi hilo lote liligharamiwa na ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma na kwamba jambo hilo limechochea kwa kiasi kikubwa siasa za maridhiano zinazoelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya viongozi wa vyama vya siasa, Ramadhani Songoro alisema kuwa Mkuu huyo wa mkoa ameona umuhimu wa viongozi wa vyama vya siasa kushiriki zoezi hilo na kufanikisha zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa.
Kwa upande wake Katibu wa Kamati hiyo, Rajabu Ambalu ambaye ni Katibu wa Chama cha NCCR – Mageuzi mkoa Kigoma alisema kuwa zoezi la uhamasishaji daftari la wakazi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa limewaweka Pamoja viongozi wa vyama vyote vya siasa na kufanya kazi kwa maslahi ya wananchi.
Pamoja na hivyo amewataka viongozi wa vyama vya siasa kufuata taratibu za kuchukua na kurudisha fomu huku akitaka busara kutumika kunapokuwa na makosa kwenye fomu za wagombea ili ziweze kurekebishwa badala ya kuonekana hazifai
Akizungumza katika mkutano huo MKUU wa mkoa Kigoma Thobias Andengenye amesema kuwa viongozi wa vyama vya siasa wamefanya kazi kubwa ya hamasa kwa wananchi iliyoweza kufanikisha wananchi wengi kujitokeza kushiriki katika zoezi la uandikishaji wapiga kura katika daftari la wakazi kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa kazi ya uhamasishaji waliyofaanya kwa kutembea mkoa mzima imewezesha mkoa kushika namba sita katika uandikishaji wapiga kura katika zoezi hilo na kufikisha asilimia 99.7 ya uandikishaji.
Andengenye alisema kuwa jambo ni jambo kubwa linapaswa kupongezwa na kwamba baada ya kazi hiyo sasa limeanza zoezi lingine la wagombea kutoka kwenye vyama kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali hivyo viongozi hao wa vyama vya siasa wanalo pia jukumu la kuhamasisha wanachama wao kuchukua na kurudisha fomu kwa amani ili kufaanikisha mchakato huo wa uchaguzi wa kidemokrasia.
0 Comments