Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Dkt. Thomas Masanja (kushoto)akihojiwa na mtangazaji Francis Godwin katika kipindi Cha Tanzania ya Leo kupita studio za Matukio Daima media kuhusu Majukumu ya tume ya Haki za binadamu na utawala Bora picha na Matukio Daima media
Na Matukio Daima media,Iringa
KAMISHNA wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Dkt. Thomas Masanja, amesema kuwa tume hiyo haijapokea malalamiko rasmi yanayohusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu au utawala bora katika zoezi la uandikishaji wapiga kura.
Uandikishaji huo ulianza tarehe 11 Oktoba na kukamilika tarehe 20 Oktoba mwaka huu, ambapo takriban asilimia 81.15 ya wananchi walijitokeza kujiandikisha.
Akizungumza katika kipindi cha Tanzania Leo kinachorushwa na Matukio Daima chini ya uongozi wa Francis Godwin, Dkt. Masanja alibainisha kuwa hakuna taarifa zozote rasmi zilizopokelewa kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu katika zoezi hilo.
Aidha, aliwapongeza Watanzania kwa kujitokeza kwa wingi na kuonyesha mwamko mkubwa wa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.
Dkt. Masanja alisema kuwa mafanikio haya yanatokana na elimu ya haki za binadamu ambayo imeendelea kutolewa kupitia majukwaa mbalimbali, yakiwemo vyombo vya habari.
Alisisitiza kuwa mwamko huu unaonyesha kuwa Watanzania sasa wanatambua haki yao ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa.
> "Jamii imekuwa na mwamko mkubwa na sasa watu wanajua maana ya haki zao za binadamu na utawala bora.
Asilimia 81.15 ya waliojiandikisha ni mafanikio makubwa wale ambao hawakujiandikisha labda walikumbwa na changamoto za kibinadamu," alisema Dkt. Masanja.
Akizungumza haki ya Kuchagua alisema ni Msingi wa Amani na Utulivu katika Taifa .
Hivyo alisema kuwa jamii inapotambua haki ya uchaguzi, migogoro inapungua kwa kuwa kila mmoja anaheshimu nafasi yake.
Aliongeza kuwa Tume ya Haki za Binadamu huanza kufuatilia utekelezaji wa haki hizi kuanzia hatua za awali za uandikishaji ili kuhakikisha kuwa hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora.
Katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, tume hiyo imekuwa ikitoa elimu na ushauri ili kuimarisha chaguzi huru na za haki.
Dkt. Masanja alifafanua kuwa ikiwa kutatokea changamoto zozote katika uchaguzi wa mitaa au uchaguzi mkuu, tume itatoa taarifa na ushauri kwa mamlaka husika, ikiwemo Tume ya Uchaguzi.
Hata hivyo alisema Kukataza Mtu Kushiriki Uchaguzi ni Kosa Kisheria hivyo alisema kuwa kumzuia mtu kushiriki uchaguzi ni kosa la kisheria, kwa sababu hiyo ni haki ya msingi ya kila raia.
Alisema kuwa vyama vya siasa vina mamlaka ya kumzuia mtu asishiriki uchaguzi kulingana na katiba na vigezo walivyojiwekea.
"Kama mtu binafsi anachagua kutoshiriki kupiga kura, hilo ni uamuzi wake binafsi na si kosa. Lakini kushawishi au kumzuia mtu mwingine asiende kupiga kura ni kosa," alieleza Dkt. Masanja.
Akizungumzis ushirikiano wa Tume na Ofisi za Utawala Dkt. Masanja alibainisha kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inashirikiana na ofisi za utawala, kama ofisi za mkuu wa mkoa na katibu tawala, ili kusimamia haki za binadamu na kuhakikisha utawala bora unatekelezwa ipasavyo.
Tume hiyo pia imeanzisha mkakati wa kufika mikoani kutoa elimu ya haki za binadamu na utawala bora, hasa katika maeneo ambako ukiukwaji wa haki umeonekana kuwa mkubwa.
"Tumeanza na mikoa yenye idadi kubwa ya watu na yenye changamoto kubwa za haki za binadamu. Baadaye tutafika katika mikoa mingine, ikiwemo Iringa," alisema Dkt. Masanja.
Katika hatua nyingine Dkt Masanja alisema tume imeendelea kutoa Elimu ya Haki na Utawala Bora kwa jamii nchini.
Kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa serikali, tume itafika vijijini na mikoani kuendeleza utoaji wa elimu.
Alisema tume itashirikiana na vyombo vya habari, asasi za kiraia, viongozi wa dini, na wanasiasa ili kufikisha elimu ya haki za binadamu na utawala bora kwa jamii.
TAZAMA MAHOJIANO YOTE HAPA
0 Comments