Na MWANDISHI MATUKIO DAIMA APP
SEREKALI ya Mapindizi ya Zanzibar imesema inaendelea na juhudi mbali mbali za kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi ili kuhakikisha nchi inakua salama.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Harusi Said Suleiman alisema hayo alipokuwa akizungumza na wadau wa mazingira katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi katika ukumbi wa Shekhe Idrisa Abdul Wakili Kikwajuni Zanzibar.
Alisema Zanzibar ni miongoni mwa nchi iliyoathirika na mabadiliko hayo katika nyanja mbali mbali ikiwemo za kiuchumi na kijamii.
“Sehemu kubwa zilizoathirika katika maeneo hayo ni pamoja na kilimo, uvuvi, utalii na makaazi ya wananchi hali ambayo kwa namna moja au nyengine imesababisha kurudisha nyuma juhudi za wananchi na taifa kwa ujumla katika kukuza uchimi wa nchi,”alisema.
Alisema mwaka 2012, Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais ilifanya utafiti ulionyesha kuwa hali ya hewa ya Zanzibar imeathirika kutokana na mabadiliko ya Tabianchi jambo lilosababisha kupanda kwa joto na mvua kubwa zinazosababisha majanga.
Aidha alifahamisha kuwa kutokana na hali hiyo serikali itahakikisha inapambana katika kupunguza na kuzuia atahari hizo ili kuona nchi haiathiriwi na mabadiliko hayo kama vile kujenga matuta katika sehemu zilizoathirika kama vile Kilimani kwa Unguja na Kojani,Mzingani,na Sipwese kwa Pemba.
“Miaka 30 iliyopita wastani wa kiwango cha juu cha joto kimeanda na kuanza kufikia nyuzi 39 na kusababisha majanga, ambapo Zanzibar maeneo 148 yameathirika, 125 Pemba na 23 Unguja,” Waziri Harusi.
Hivyo aliwasisitiza wadau wa mazingira kushirikiana na serikali katika kutoa elimu kwa wananchi ili kuona athari hizo zinaendelea kulindwa ili kuweka ustawi mzuri wa taifa.
Mkururugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Mazingira Zanzibar (ZACCA) Mahafudhi Shaaban Haji alisema lengo la mkutano huo ni kuiunga mkono serikati katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo jumuiya hiyo itahakikisha Zanzibar inakua ya kijani katika kuleta maendeleo ya kimazingira nchini.
“Serikali kuangalia uwezekano wa kufanya mkutano huo kila mwaka ili kuongeza uwelewa kwa jamii na taifa kwa ujumla katika kupunguza na kudhibiti athari za kimazingira ambapo Zanzibar kuna uharibifu mkubwa wa kimazingira,” Mahfoudh.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo Mkururugenzi Mkuu Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Sheha Mjaja Juma, alisema miongoni mwa athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na utupaji wa taka hali ambayo inachangia uharibifu mkubwa wa mazingira katika sehemu mbali mbali ikiwemo za kiuchumi, kijamii na maeneo mengine.
Hivyo alizitaka jamii na wadau wa mazingira kuendelea kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti na kuacha kufanya uharibifu wa mazingira katika makaazi ya watu na maeneo ya kiuchumi ikiwemo bahari na hifadhi za misitu.
Afisa mradi wa Mabadilko ya Tabianchi (ZANZIADOPT) kutoka Chama cha Waandishi wa habari Wanawawake Tanzania, TAMWA ZNZ Nayrat Abulla Ali alisema mabadiliko ya tabianchi ni jambo linalomuhusu kila mmoja, hivyo ameiasa jamii kushirikiana kwa pamoja kuyatunza mazingira.
Makamo Mwenyekiti wa Bodi ya watoto Tanzania ambae pia ni Balozi wa Mazingira Zanzibar Muhsin Haji ameiomba Serikali kuimarisha club za watoto na kutoa elimu jinsi gani watoto wanaweza kujilinda katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
Washiriki wa mkutano huo walisema athari za mabadiliko ya tabianchi zinawaathiri zaidi kina mama na watoto hasa wa vijijini kwa kukosa hewa safi,lishe bora pamoja na ukosefu wa nishati isiyo salama ya kupikia.
Walisema athari nyengine pia zinawaathiri zaidi wavuvi na wakulima wa mwani kwa kupoteza ajira zao na kushuka kipato chao siku hadi siku.
Mkutano huo wa siku tatu ulioandaliwa na Taasisi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, (ZACCA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamo wa kwanza wa Rais Zanzibar, umewashirikisha wadau wa mazingira wakiwemo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA ZNZ, na kuhudhuriwa na washiriki 250 wa ndani na nje ya Zanzibar ambapo mada 15 zinazohusiana na masuala ya uhifadhi, athari na mikakati ya kitaifa na kimataifa zitawasilishwa.
0 Comments