Na Matukio Daima Media , Simiyu.
WAKALA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mkoani Simiyu imetekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Madaraja na Barabara katika Wilaya, Halmashauri, Kata na Vijiji vya Mkoa huo.
Ujenzi huo umeongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi na kuchochea maendeleo ikiwemo ukuzaji wa fursa za Biashara pamoja na kurahisisha Usafiri na Usafirishaji wa bidhaa na mazao.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Gaston Paschal wakati wa mahojiano maalum yaliyofanyika ofisini kwake.
Mhandisi Gaston amesema miradi hiyo inachochea ukuaji wa Uchumi na kwamba inagusa maisha ya wananchi hasa wakulima na wafugaji.
“Katika utekelezaji wa miradi yetu, tuna miradi ya kimkakati, ambayo inagusa wananchi moja kwa moja, na unakuta ilikuwa ni kilio cha siku nyingi katika maeneo yao,” amesema Mhandisi Gaston.
Amesema kuwa katika Wilaya ya Busega kulikuwa na changamoto kati ya Kata ya Mwamanyili na Kata ya Nyaluhande kutokana na mto uliotenganisha kata hizo mbili ambayo sasa umepatiwa ufumbuzi.
Ameeleza kuwa TARURA imefanikiwa kujenga daraja la Mwamanyili lenye upana wa mita 20, na kuwezesha wananchi kupita kutoka kata moja kwenda nyingine bila changamoto yoyote.
Kwa Wilaya ya Bariadi, Mhandisi Gaston amesema TARURA imekamilisha ujenzi wa daraja la Mwadobana lenye urefu wa Mita 36, ambalo limeunganisha kata nne katika wilaya hiyo.
Na katika Wilaya ya Itilima, Mhandisi Gaston amesema, TARURA inatekeleza ujenzi wa barabara ya KM 5.2 ambayo inagharimu shilingi bilioni 3.4, ujenzi huo unatumia teknolojia mbadala ya Ecoroads.
“Barabara hii inakwenda Hospitali ya Wilaya ya Itilima, hivyo itakapokamilika itakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Itilima, hasa kwa wagonjwa wanaokwenda kupata matibabu katika hospitali ya wilaya,” amesema Mhandisi Gaston.
Ameendelea kusema kuwa, kwa Wilaya ya Maswa kulikuwa na shida ya maji kufurika na tope kujaa katika eneo la Mji wa Maswa, ambapo mwaka jana TARURA imefanikiwa kujenga barabara ya lami Kilometa 1 na kuweka taa katika eneo hilo korofi.
“Upande wa Meatu tunajenga daraja la Mwanzagamba kwa kutumia teknolojia rahisi, lenye upana wa Mita 25, ambalo limekamilika na linaunganisha kata tatu,” amesema Mhandisi Gaston.
Amesema, miradi hiyo imebadilisha muonekano wa mtandao wa barabara mkoani humo, ambapo kulikuwa na barabara nzuri zinazopitika asilimia 22, kwa sasa zimefikia asilimia 46 na barabara zisizoridisha zimepungua kutoka asilimia 36 hadi asilimia 18.
0 Comments