Na Matukio Daima media,Simiyu
KATIBU Tawala wa Mkoa wa Simiyu Prisca Joseph Kayombo ametembelea na kuwahimiza watumishi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoani humo kwenda kujiandikisha kwenye Daftari la wakazi ili waweze kupata haki yao ya Msingi ya kuchagua Viongozi wa serikali za Mitaa.
Akizungumza na watumishi hao kwenye Ofisi zao zilizopo Kata ya Malambo, katika muendelezo wa zoezi la kuhamasisha makundi mbalimbali Mkoani Simiyu kujitokeza kujiandikisha, Katibu Tawala huyo amesema Uchaguzi huo wa serikali za Mitaa utafanyika Nov 27, 2024.
Amewataka watumishi hao kutochanganya zoezi la maboresho ya Daftari la kudumu la Wapiga kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu na Daftari la wapiga kura za viongozi wa Serikali za Mitaa.
Amewataka pia kuwa mabalozi wa kuhamasisha Wananchi kujitokeza katika vituo vya kujindikisha ili waweze kuwa na sifa ya kupiga kura kuwachagua Viongozi wa Serikali za Mitaa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI uchaguzi wa Serikali za Mitaa Nchini utafanyika Tarehe 27 Novemba 2024.
0 Comments