NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi ameendelea na ziara ya kikazi katika Kata ya Uru Kaskazini akiambatana na Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhani Mahanyu, Katibu wa UWT Wilaya ya Moshi Vijijini Oliver Ngalawa, Diwani wa Kata, Miriam Msoka, Viongozi wa CCM Kata ya Uru Kaskazini na wataalamu kutoka MUWSA.
Katika ziara hiyo alitembelea vijana wa bodaboda na kuongea nao na pia alikagua miradi ya maendeleo katika Shule za Msingi za Ngasini na Msareni.
Katika shule ya Msingi Msareni Mbunge alitembelea ujenzi wa Choo cha walimu ambapo mfuko wa Jimbo umetumika kutekekeza mradi huo kwa kupeleka jumla ya shilingi milioni 7,452,100 pia alijionea uharibufu wa tenki la maji lililojengwa kwa mbao katika kijijiji cha Mrawi.
Mbunge akiwa katika mkutano wa hadhara, aliwaeleza wananchi kuwa kwa kipindi cha miaka minne tokea aingie madarakani, serikali imetoa fedha nyingi kutekeleza miradi ya maendeleo katika Kata ya Uru Kaskazini.
Miradi mbalimbali imetekelezwa katika maeneo ya Elimu, Miundombinu ya Barabara, Mikopo kwa vikundi, Kilimo, Maji, Umeme, na kudai kuwa katika kipindi cha ubunge wake kwa miaka minne iliyopita, Kata hiyo imepokea kiasi cha shilingi bilioni 1,688,108,194.00
Katika mkutano huo wa hadhara, wananchi walieleza kero mbalimbali zinazowakabili zikiwemo ubovu wa barabara zote za ndani zinazohudumiwa na TARURA katika Kata ya Uru Kaskazini na kutolea mifano ta barabara za KNCU - Kisarika, barabara ya Sokoni - Njari inayojulikana kama barabara ya Mandela, barabara ya Wami Ngomberi Estate, Daraja la Mbora, na barabara ya mama mbuzi.
Wananchi walilalamika kwamba TARURA wamekuwa wanafanya ujenzi wa barabara katika maeneo ya Uru Kaskazini bila kuwashirikisha viongozi wa maeneo husika wala wananchi.
Kwa upande wa kilimo, wananchi waliomba ufanyike ukarabati wa uhakika wa mifereji ya asili hasa ile ya Ongoma Okaseni, Rau Mtiro na Ngoromu ambapo kwa ujumla Serikali imeshapeleka shilingi milioni 12,567,594.00 katika Kata ya Uru Kaskazini kukarabati mifereji ya asili.
Baadhi ya wananchi waliibua hoja kwamba kuna baadhi ya kaya maskini zimenyimwa fursa kunufaika na miradi wa TASAF na kumwomba Mbunge awasaidie ili kero hii itatuliwe.
Katika mkutano wa Mbunge, baadhi ya wananchi walilalamika kwamba hakuna uwazi kutoka kwa viongozi kwa ruzuku inayotolewa na waliokodisha mashamba ya vyama vya ushirika vya Uru Kaskazini (Machare na Uru Estate) kwenye ubia wa joint ventures.
Walilalamika kwamba, kuna mianya mikubwa sana ya ufujaji wa fedha za ushirika huo na Mbunge alimuomba Mwenyekiti wa CCM Kata afuatilie na ampe taarifa kamili kimaandishi ili alifikishe jambo hilo kwenye tume ya Ushirika Dodoma.
Kwa uchungu mkubwa, wananchi walieleza kuwa kuna uhusiano mbaya kati ya KINAPA na vijiji vinavyopakana na mlima Kilimanjaro ambapo walisema, akina mama hawaruhusiwi kwenda kukata majani ya mifugo wala kuokota kuni za kupikia pia wananchi walikuwa wanapata vikwazo kutoka KINAPA walipoomba vibali kwenda kukarabati vyanzo vya maji vilivyopo katika msitu wa mlima Kilimanjaro.
Mwananchi mmoja alitoa ombi kwa Mbunge asaidie kufuatilia swala la matibabu ya wazee, kwani wengi wao hawana fedha za kuwatibu ambapo Prof. Ndakidemi alisema kwamba Serikali inaendelea na zoezi la utambuzi na kuwapatia wazee vitambulisho, na lengo ni kuwapatia wazee wote nchini vitambulisho hivyo ili wapate huduma bora ya matibabu.
Kwa ujumla wake, Mbunge alijibu kero zote zilizoibuliwa na wananchi. Na zile kero ambazo hazikuwa na majibu alizichukua na kuwahakikishia wananchi kuwa atazipeleka kwenye mamlaka husika.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu na wa UWT Wilaya, Oliver Ngalawa kwa nyakati tofauti walitoa pongezi nyingi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika kata ya Uru Kaskazini.
Wamewataka wananchi wa Uru Kaskazini kuendelea kumuunga mkono Rais, Mbunge na Diwani kutokana na kazi nzuri walizofanya.
Mwisho.
0 Comments