Header Ads Widget

MBUNGE NJEZA AWATUNUKU VYETI WAHITIMU 248 JUHUDI SEKONDARI, AHIMIZA ELIMU.

NA JOSEA SINKALA, MBEYA.

Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza, amewahimiza wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao akisema elimu ndio utajiri na mkombozi wa mtoto.

Mbunge Njeza amesema hayo wakati akizungumza na wazazi, walezi na wanafunzi katika shule ya sekondari Juhudi Usongwe, mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi kwenye mahafali ya kwanza ya kuwaaga wanafunzi 248 wa kidato cha nne wanaotarajiwa kuhitimu mwaka huu.


Mhe. Mbunge Oran Njeza, amesema elimu ndio msingi wa maendeleo hivyo Serikali itaendelea kuboresha miundombinu/mazingira ya utolewaji elimu ili wanafunzi wasome katika mazingira bora.

Akijibu risala ya wanafunzi na ile ya shule ya sekondari Juhudi, Mbunge Njeza ameitaka Halmashauri ya Mbeya kuweka kipaumbele kwenye ujenzi wa uzio wa shule hiyo ili kusaidia kupunguza utoro na kuweka usalama zaidi shuleni hapo pamoja na ujenzi wa chumba maalum kwa ajili ya TEHAMA na vitendea kazi vinginevyo huku akiahidi mfuko wa jimbo kuwaunga mkono kwenye harakati za uboreshaji miundombinu shuleni hapo.


Kuhusu uboreshaji huduma ya maji, Mhe. Mbunge ameahidi kuwasiliana na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mbeya kuona namna bora ya kuboresha huduma kwenye shule hiyo changa.


Akitoa taarifa ya shule ya sekondari Juhudi Usongwe, mkuu wa shule hiyo mwalimu Victoria Somola, amesema shule yake ilianza kujengwa mwaka 2020 na kusajiliwa rasmi mwaka 2021 na kitaaluma inafanya vizuri, hivyo kumuomba Mbunge na Serikali kuendelea kuwaunga mkono ili kuhakikisha inakuwa miongoni mwa shule bora mkoani Mbeya na Tanzania kwa ujumla.


Pamoja na mengineyo, mwalimu Somola ameomba kujengewa uzio shuleni hapo ili kuzuia utoro, kujengwa jengo la utawala na kuboresha eneo la vifaa vya maabara na kuwashukuru wazazi na walezi wanaochangia chakula shuleni jambo linalochochea ari ya watoto kutulia shuleni kwa ajili ya masomo.

Kwa upande wake afisa elimu taaluma wilayani Mbeya Mwalimu Stanley Mwasi, amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya kutolea elimu kwa kuhakikisha fedha zinaendelea kutolewa kwenye shule mbalimbali pamoja na ujenzi wa shule mpya na kumshukuru mbunge kwa kuendelea kuomba fedha Serikalini.

Mahafali hayo yamehudhuriwa na jeshi la Polisi kitengo cha dawati la jinsia na watoto wilaya ya kipolisi Mbalizi, ambapo mkuu wa dawati hilo Inspector Mary Gumbo, ameitaka jamii kushirikiana ili kukomesha matukio ya ukatili na unyanyasaji ikiwemo kwa watoto ili kuwasaidia kutimiza ndoto zao.


Insp. Mary Gumbo, amesema ni vizuri wazazi na walezi kuzungumza na watoto wao wa jinsi zote juu ya mwenendo wa Dunia ili kutoharibiwa na utandawazi ikiwemo kutojihusisha na matendo ya jinsi moja na kwamba ndio maana jeshi la Polisi kote nchini limekuja na kampeni ya tuseme nao kabla hawajaharibiwa.


Baadhi ya wananchi waliozungumza na kituo hiki, wanasema ushirikiano unahitaji baina yao na Serikali kuhakikisha watoto wanalelewa vema ili kuwalinda na matukio ya uhalifu, ukatili na unyanyasaji na kuwafanya watimize ndoto zao.






Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI