NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Jeshi la Polisi kupitia dawati la jinsia na watoto wilaya ya kipolisi Mbalizi, limeitaka jamii kushirikiana kukomesha matukio ya ukatili na unyanyasaji ikiwemo kwa watoto ili kuwasaidia kuhakikisha wanatimiza ndoto zao.
Hayo yameelezwa na mkuu wa dawati la jinsia na watoto wilayani humo Inspector wa Polisi Mary Gumbo, wakati akizungumza na wazazi, walezi na wanafunzi katika shule ya sekondari Juhudi Usongwe, kwenye mahafali ya kwanza ya kuwaaga wanafunzi 248 wa kidato cha nne.
Amewataka wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanashirikiana kutoa malezi bora kwa watoto wao na kuwalinda na vitendo mbalimbali vya ukatili na unyanyasaji.
Amesema ni vizuri wazazi na walezi kuzungumza na watoto wao wa jinsi zote juu ya mwenendo wa Dunia ili kutoharibiwa na utandawazi ikiwemo kutojihusisha na matendo ya jinsi moja na kwamba ndio maana jeshi la Polisi kote nchini limekuja na kampeni ya tuseme nao kabla hawajaharibiwa.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na kituo hiki, wanasema ushirikiano unahitaji baina yao na Serikali kuhakikisha watoto wanalelewa vema ili kuwalinda na matukio ya uhalifu, ukatili na unyanyasaji na kuwafanya watimize malengo huku wakimweka Mungu kuwa namba moja.
Kwa upande wake afisa elimu taaluma wilayani Mbeya Mwalimu Stanley Mwasi, amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha miundombinu ya kutolea elimu kwa kuhakikisha fedha zinaendelea kutolewa kwenye shule mbalimbali pamoja na ujenzi wa shule mpya.
Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza, ameahidi ushirikiano na shule hiyo pamoja na kuendelea kuiomba Serikali kutoa fedha ili kuboresha miundombinu ya shule hiyo.
0 Comments