Header Ads Widget

MAKALA :VYAMA VYA SIASA,FAMILIA,JAMII PANDE TATU ZENYE MAONI TOFAUTI KWA WANAWAKE KUSHIKA NAFASI ZA UONGOZI

 

Na Thabit Madai,Zanzibar- Matukio Daima App

UONGOZI ni ushawishi, dhana na taaluma inayompa mtu madaraka ya kuongoza ili kuleta maendeleo katika eneo ambalo anataka kuliongozi, Juhudi za wanawake kuwa viongozi Zanzibar  bado kitendawili kutokana kuwa wanawake hao wanakabiliana na changamoto nyingi  kama vile,rushwa ngono, mila na desturi kandamizi, kutoungwa mkono katika familia,jamii na vyama vya siasa.


Ripoti ya Maalumu ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 iliyotolewa na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar – TAMWA –Z inaeleza kuwa, Wanawake viongozi Zanzibar ni asilimia 36 tu ambapo wawakilishi ni nane katika majimbo 50 ya uchaguzi, wabunge wanne, Mawaziri Sita sawa asilimia 33, makatibu wakuu saba sawa asilimia 39, Mkuu wa mkoa Mmoja sawa na asilimia 20, wakuu wa wilaya wanne sawa na asilimia 36.

Khairia Mohammed, 28 mkaazi Mwembetanga Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, alikuwa mgombea wa nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Malindi Unguja, Simulizi yake ya kipekee inaeleza moja ya sababu iliyomkwamisha kufikia mbali katika safari yake ya uongozi ni pamoja a kutoungwa mkono na familia na hata jamii.


"Baada ya kujiona nina uwezo mkubwa wa kuwa kiongozi niliamua kugombea nafasi ya Ubunge Jimbo la malindi kupitia Chama Cha Mapinduzi - CCM lakini mchakato haukuwa rahisi kwani nilikumbana na changamoto nyingi ambazo zilianzia katika familia yangu ambao wao walikuwa hawaamini kabisa kama nina weza kuwa kiongozi,"Amesema Khairia.

Harakati zake za siasa na uongozi zilianza mwaka 2016 alikuwa Waziri wa Michezo,Sanaa na Utamaduni lakini pia wakati yupo chuoni aliteuliwa  kuwa Mwenyekiti wa Elimu na Mikopo katika Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar –ZAHLFE. Baadae aligombea na kuchaguliwa kuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi CCM -UVCCM.


Ameongeza kuwa, "Mtazamo wa baadhi ya  wanafamilia yangu kuwa kiongozi mwanamke ni uhuni hivyo nilikosa mashirikiano pale ambapo nilikuwa nahitaji msaada kutoka kwao jambo ambalo lilipelekea kushindwa kufikia malengo yangu na kuwa kiongozi," Amemalizia Khairia.


"Jamii inayotuzunguka kiukweli wanaona Wanawake kujihusisha na masuala ya kisiasa ni uhuni jambo ambalo si kweli uhuni ni mtu yeye mwenyewe kujiheshimu na kujua nini anataka, kwa Mwanamke yoyote anaetaka kuingia katika Siasa ushauri wangu awe na chanzo cha kumuingizia kipato ili asiwe ombaomba au kutumiwa kwa sababu hana kitu," amefafanua.


Sensa ya Watu na Makaazi ya Zanzibar ya mwaka 2022 inaonesha kuwa Zanzibar ina watu 1,889,773 kati ya hao Wanawaume ni 915,492 na Wanawake 974,291 hii inamana kwamba,Wanawake ni asilimia 51.6 ya wakaazi wa Zanzibar.


Licha ya wingi huo bado kumekuwa na upungufu wa Wanawake kushiriki katika uongozi kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa uungwaji mkono ndani ya vyama, Familia na katika jamii.


Almas Ali Mohammed ni Mchambuzi wa masuala ya kisiasa visiwani Zanzibar anaeleza kuwa, kukosekana kwa uungwaji mkono kwa wanawake ndani ya vyama vya siasa, familia na hata jamii ni moja ya changamoto inayorudisha nyuma wanawake wengi kukosa kufikia malengo yao ya kuwa viongozi.


"Ukweli kuwa wanawake katika uongozi wanakabiliwa na changamoto nyingi ila kubwa zaidi ni kukosa uugwaji mkono na hii inasababishwa na jamii husika kuwa mitazamo potofu ya kuwa wanawake hawawezi kuongoza," Amesema Almas huku akisema wakati mwengine familia na jamii inawakubali wanawake ila vyama vinakuja kuwaondoka kwenye vinyang’anyiro vya uchaguzi. 


Katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 mchakato wa kuwania nafasi za uongozi kwa majimboni ulihamasika mno kiasi kwamba wanawake zaidi ya 300 walijitokeza kwenye vyama mbalimbali vya siasa hususani vile vyenye ushindani mkubwa.


Katibu wa Kamati maalum ya Halmashauri kuu Taifa- NEC ya Chama cha Mapinduzi CCM Idara ya Itikadi na Uenezi Khamis Mbeto amekiri kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake katika kuwania nafasi za uongozi “Familia ikubali na iwaruhusu lakini pia changamoto ya ndani ya vyama nayo ni suala ambalo tunaliangalia”Amemaliza Mbetto.


Sheria ya vyama vya siasa nchini namba No.5 ya mwaka 1992, sura ya 258 inaweka sharti kwa vyama vya siasa nchini kuhakikisha usawa wa kijinsia katika kuandaa na kutekeleza sera zake. 


Utafiti uliofanyika mwaka 2013 uliofanyika na wadau kutoka vyama 16 vya siasa nchini Tanzania pamoja na wanasheria umebaini kuwa bado kuna changamoto ya utekelezaji wa sheria hiyo kutokana na baadhi ya vyama vya siasa kutoweka mazingira wezeshi wagombea wanawake.


Thabit Idarous Faina ni Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar - ZEC amekiri kuwepo kwa changamoto zinazowakabili wanawake kufikia nafasi ya uongozi huku akieleza kuwa Tume ina sera jumuishi ya jinsia ambayo inalenga kuhamasisha jinsia zote kugombea nafasi mbalimbali za uongozi."Ni vyema sana viongiozi wa vyama vya siasa kujua umuhimu wa sera na kutoa nafasi kwa wanawake iwapo wanaons au kuhisi hawatendewi haki basi watoe taarifa na sisi ZEC tutatoa msaada," amesema faina.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI