Chifu Adam Abdul Sapi Mkwawa (kushoto )akimsikiliza kwa makini Mhifadhi mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha Iringa Godwell Meing'ataki kuhusu kukauka kwa mto Ruaha mkuu Jana wakati wa ziara ya Chifu Mkwawa na Baraza lake la wazee Waliofanya ziara ya kitalii katika Hifadhi hiyo kama sehemu ya uzinduzi wa maadhimisho ya Miaka 60 ya Hifadhi ya Ruaha yaliyoanza Tarehe 1-7 mwezi Oktoba picha na Matukio Daima App
Na Matukio Daima App
CHIFU Adam Abdul Sapi Mkwawa, kiongozi wa kabila la Wahehe mkoani Iringa anayechukizwa na vitendo vya uharibifu wa mazingira unaofanywa na baadhi ya wananchi wanaoendesha shughuli za kibinadamu pembezoni mwa mto Ruaha mkuu ambao ni tegemeo kubwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Chifu Mkwawa anatoa wito kwa wananchi hao hasa wale wanaotegemea Mto Ruaha Mkuu, kuhakikisha wanatunza na kulinda chanzo hicho muhimu cha maji.
Katika kuadhimisha Miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha,maadhimisho yaliyoanza Oktoba 1-7 mwaka huu Chifu Mkwawa na Baraza lake la wazee alifanya ziara ya utalii wa ndani katika Hifadhi hiyo kubwa ya pili nchini Tanzania kama kuhamasisha utalii wa ndani pia Kwa ajili ya ujifunza mambo kadha wa kadha kwenye Hifadhi hiyo .
Baada ya kuingia lango kuu la Hifadhi majira ya saa 5:45 asubuhi ya Jumanne Oktoba 1 mwaka huu analazimika kushuka daraja la Mto Ibuguziwa ambalo linakuvusha hadi ndani ya Hifadhi hapa anasimama na kuulilia mto Ruaha mkuu ambao wanyama wa majini kama viboko na mamba wakihangaika kwa jua kutokana na kina kifupi Cha maji ya madimbwi kilichosalia eneo hilo.
Chifu Mkwawa anasema kuwa Mto Ruaha Mkuu una umuhimu mkubwa si tu kwa wanyamapori waliomo ndani ya hifadhi, bali pia kwa jamii ya watu wa Iringa, ambao wameutegemea mto huo kwa miaka mingi kama chanzo kikuu cha maji kwa matumizi ya nyumbani, kilimo, na ufugaji.
Chifu Mkwawa anabainisha kuwa ni muhimu sana kwa jamii zinazoishi pembezoni mwa hifadhi kuchukua jukumu la moja kwa moja katika kulinda na kuhifadhi mazingira ya Mto Ruaha Mkuu, kwani mto huo si mali ya hifadhi pekee, bali ni urithi wa wote.VIDEO:ZIARA YA CHIFU MKWAWA NA BARAZA LAKE LA WAZEE
Mkwawa anaitumia nafasi hiyo kuipongeza serikali ya awamu ya sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuboresha miundombinu ya barabara na kiwanja Cha ndege katika kuboreshwa sekta ya utalii mkoani Iringa.
Anasema kuwa kazi kubwa iliyofanywa katika kuboresha Uwanja wa Ndege wa Iringa na Uwanja wa Ndege ndani ya Hifadhi itasaidia kuleta watalii wengi zaidi hifadhini, na pia ujenzi wa barabara ya Iringa - Msembe ambayo imeongeza urahisi wa kufikia hifadhi hiyo.
Kwa mujibu wa Mkwawa, miundombinu hiyo imekuwa kichocheo muhimu katika kukuza sekta ya utalii mkoani Iringa na nchi nzima kwa ujumla.
Pamoja na pongezi hizo, Mkwawa anakemea vikali vitendo vya ujangili vinavyofanyika ndani ya hifadhi.
Anasema kuwa ujangili si tu unahatarisha maisha ya wanyamapori, bali pia unadhoofisha juhudi za uhifadhi na maendeleo ya utalii.
Hivyo anatoa wito kwa serikali na wananchi kushirikiana katika kupambana na ujangili kwa kutumia mbinu shirikishi, ikiwemo utoaji wa taarifa za uhalifu na uhamasishaji wa jamii kuhusu athari za ujangili.
Gerald Malangalila mwenyekiti wa baraza la mila na desturi ya Kihehe mkoani Iringa, aliunga mkono kauli ya Chifu Mkwawa, akiongeza kuwa matumizi mabaya ya maji ya Mto Ruaha Mkuu yanaweza kuleta madhara makubwa kwa wanyama na watu.
Anasema kuwa ukame na kupungua kwa maji ya mto ni tishio kwa ustawi wa hifadhi hiyo na maisha ya vijiji vinavyopakana nayo.
Malangalila anatoa rai kwa jamii kuwa na utaratibu endelevu wa matumizi ya maji ili kuhakikisha mto huo unaendelea kutiririka kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Godwell Ole Meing’ataki,mbali ya kuwapongeza Chifu Mkwawa na kundi lake kwa furaha, na akatumia fursa hiyo kuelezea historia ya hifadhi hiyo.
Meing'ataki alisisitiza kuwa Hifadhi ya Ruaha inayo historia ndefu ya uhifadhi, na kwamba mafanikio yake kwa kiasi kikubwa yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya hifadhi na jamii zinazozunguka.
Aliwahakikishia wageni kwamba usalama wao ni wa kipaumbele, na akasisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha amani kati ya binadamu na wanyamapori.
Meing’ataki pia alizungumzia jitihada za hifadhi katika kuboresha huduma za watalii, zikiwemo uboreshaji wa malazi na vivutio vingine vya utalii ndani ya hifadhi.
Alisema kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha inabakia kuwa kivutio kikubwa cha utalii nchini, huku ikidumisha viwango vya juu vya uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.
Katika hitimisho la ziara hiyo, Chifu Mkwawa alisisitiza kuwa jukumu la kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji ni la kila mmoja, na kwamba juhudi za serikali pekee hazitoshi.
Alitoa wito kwa wananchi wote wa Iringa na Tanzania kwa ujumla kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kulinda vyanzo vya maji kama Mto Ruaha Mkuu, kwa kuwa ni hazina ya taifa. Pia aliwaomba viongozi wa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira, hasa maji, kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi na kijamii.
Ziara ya Chifu Mkwawa na wazee wa kabila la Wahehe inadhihirisha umuhimu wa urithi wa kitamaduni na kimazingira unaopaswa kuhifadhiwa na kizazi cha sasa na kijacho.
Mto Ruaha Mkuu, kama ilivyo kwa vyanzo vingine vya maji nchini, ni chanzo cha uhai kwa wanyama na binadamu, na kulinda mto huo ni kulinda maisha ya wengi.
Wito wa Mkwawa ni kumbukumbu ya umuhimu wa uwajibikaji wa jamii katika masuala ya uhifadhi, hususan katika maeneo ya hifadhi za taifa ambazo ni nguzo muhimu ya uchumi na utalii wa Tanzania.
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ikiwa ni miongoni mwa hifadhi kubwa barani Afrika, inaendelea kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi, na hivyo, jitihada za kuilinda hifadhi hii ni za lazima ili iendelee kuwa urithi wa taifa na chanzo cha maendeleo endelevu.
Wito wa Chifu Mkwawa ni mwaliko kwa jamii na wadau wote wa uhifadhi kushirikiana kwa pamoja katika kuendeleza juhudi hizi kwa ustawi wa wote.
Ikumbukwe kuwa ziara hii ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha maadhimisho yaliyoanza Oktoba 1 na kuhitimishwa Oktoba 7 mwaka huu na Waziri wa Maliasili na utalii Balozi Dkt Pindi Chana.
MAKALA HII IMEANDIKWA NA FRANCIS GODWIN MTAYARISHAJI WA MAUDHUI MATUKIO DAIMA MEDIA ANAPATIKANA KWA SIMU 0754026299 BARUA PEPE: matukiodaima3@gmail.com.
0 Comments