Header Ads Widget

HIFADHI YA SERENGETI NA MLIMA KILIMANJARO ZASHINDA TUZO BARANI AFRIKA

Taasisi ya World Travel Awards imetangaza hifadhi mbili za Tanzania kuwa washindi wa tuzo katika vipengele vya hifadhi na kivutio bora cha utalii barani Afrika kwa mwaka 2024.

 Hifadhi ya Taifa Serengeti imeshinda tuzo ya Hifadhi Bora Barani Afrika (“Africa’s Leading National Park 2024”), huku Mlima Kilimanjaro ukitangazwa kuwa Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika (“Africa’s Leading Tourist Attraction 2024”).


Tuzo hizo zilitolewa usiku wa tarehe 18 Oktoba 2024, katika ukumbi wa Diamonds Leisure Beach & Golf Resort nchini Kenya.


Akitangaza washindi, Mwanzilishi wa World Travel Awards, Bwana Graham Cooke, alisema kuwa Serengeti imepata ushindi kwa kuipita hifadhi maarufu za Afrika, ikiwemo Maasai Mara (Kenya), Kruger (Afrika Kusini), Central Kalahari (Botswana), Etosha (Namibia), na Kidepo Valley (Uganda).


Aidha, Bwana Cooke alieleza kuwa Mlima Kilimanjaro umeshinda dhidi ya vivutio vingine vya utalii vya kipekee barani Afrika kama Hifadhi ya Ngorongoro, Hartbeespoort Aerial Cableway, V&A Waterfront, Kisiwa cha Robben, Mlima Table (vyote vya Afrika Kusini), Ziwa Malawi, Delta ya Okavango (Botswana), na Piramidi za Giza (Misri).



Tuzo hizo zilipokelewa na ujumbe ulioongozwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Bw. Nkoba Mabula, pamoja na viongozi wengine, wakiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii, Bw. Ephraim Mafuru, CPA Hadija Ramadhani (Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini), Betrita Lyimo (Kamanda wa Uhifadhi, Kanda ya Kaskazini), na Stephano Msumi (Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti).


Serengeti imepata ushindi huu kwa mara ya sita mfululizo, ikiwa imebeba tuzo ya Hifadhi Bora Barani Afrika kuanzia mwaka 2019 hadi 2024. Ushindi wa mwaka huu umechangiwa na kampeni ya TANAPA ya "Vote Now," iliyofanyika kwa miezi mitatu.


Kwa upande wake, Mlima Kilimanjaro pia umefanikiwa kushinda tuzo ya Kivutio Bora Barani Afrika mara sita, katika miaka ya 2013, 2015, 2016, 2017, 2018, na sasa 2024.


Imetolewa Catherine Mbena Afisa uhifadhi mkuu kitengo Cha mawasiliano Tanapa alisema



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI