Na Mbaruku Yusuph,Matukio Daima APP Tanga.
MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendekeo (chadema) Freeman Mbowe amemuomba Rais Samia kuunda tume ya Jaji ya Kimahakama ili kuchunguza kifo cha aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chama hicho Taifa Ally Kibao.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa dua ya kumuombea Mjumbe huyo Nyumbani kwake maeneo ya Makorora Jijini Tanga kabla ya mwili wa marehemu kwenda kuzikwa katika makaburi ya nyumbani kwao maeneo ya Darigube Jijini hapa.
Mbowe alisema kila Mtanzania amesikia kauli ya Mh Rais inayoelekeza vyombo vilevile ambavyo Chadema wanaviona kuwa ndio mshitakiwa namba moja vikajichunguze vyenyewe jambo ambalo haliwezekani.
Aidha alisema njia pekee ndani ya Nchi inayaoweza kusaidia ni kuundwe tume ya Kijaji ya Kimahakama itakayoweza kufanya uchunguzi kwa kina na wale walio kuwa na ushahidi na hawahataki kuutoa kwa Jeshi la Polisi wanaweza kuwa huru kutoa ushahidi huo katika tume hiyo ya Jaji ya Kimahakama na hatua za kisheria zikachukuliwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani Hamadi Masauni kama mwakilishi wa Rais katika msiba wa Ally Mbao rai ya waombolezaji wanatambua Rais pekee ndio mwenye mamlaka ya kuunda time ya Jaji ya Kimahakama .
Alisema wananchi wanaonekana wamekasirika na ni kielelezo tosha cha tatizo jambo ambalo mliopo katika Mamlaka si rahisi kubaini machungu na magumu wanayopitia wananchi hasa wale walioumiziwa ndugu zao na ndio sababu ya amani kuyumba katika msiba huo na si ajabu amani hiyohiyo ikayumba katika mitaa mbalimbali Nchini.
"Wananchi wana maumivu ndani ya mioyo yao kutokana na viongozi wao na sio mara moja bali ni mara kadhaa wametekwa na baadhi yao kupoteza maisha,kuumizwa na wengine kupotea kusikojulikana"Alisema Mbowe
Kwa upande wake Waziri wa mambo ya Ndani Hamadi Masauni akitoa salamu za Serikali alisema Rais Samia ameguswa na msiba huo na kutokana na taarifa aliyoitoa juu ya jambo hilo kuwa lifanyiwe uchunguzi kwa haraka ili watuhumiwa wote waweze kutiwa katika mikono ya sheria.
Masauni alisema Mh Rais pamoja na Serikali yake amesononeshwa,amesikitishwa na kuumizwa sana na tukio hilo na ni jambo ambalo halikupaswa kutokea hasa katika nchi ambayo miaka yote imekuwa ikijivunia usalama na amani na kuwa nchi ya kuigwa na nchi za majirani.
Masauni aliwahakikishia waombolezaji wote hususan wanafamilia kama Serikali haitaliacha jambo hilo liende hivyohivyo na watambue melekezo ya Mh Rais yamekwisha anza kutekelezwa na hatua zitachukuliwa watakao bainika kuhusika.
Wito kwa wananchi wote kuacha kushutumu badala yake wale walio na kielelezo cha mtu kuhusika na jambo hili basi awasilishe ili hatua zaidi ziweze kusaidia kuwapata wahusika na waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) John Mnyika alisema Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka ikiwa pamoja na Waziri wa mambo ya Ndani ajiuzulu kutokana na matukio ya namna hiyo kujitokeza mara kwa mara bila hatua zozote kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao.
Mnyika alisema Chadema imepata pigo kubwa la kuondokewa na kada huyo wa Chama hicho marehemu Ally Kibao ambae alikuwa nguzo na mhimili kwa Chama hicho.
Alitumia fursa hiyo kuwaomba wanafamilia wa marehemu wawe watulivu hasa kipindi hili kigumu ambacho wameondokewa na Mzee wao wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kutafuta njia za kuwabaini wahusika wa tukio hilo.
0 Comments