Header Ads Widget

MBEYA MJINI INAHITAJI KIONGOZI MWENYE AKILI NA TUMEMPATA: UVCCM MBEYA MJINI

 


NA JOSEA SINKALA, MBEYA.


Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi CCM (UVCCM) wilaya ya Mbeya mjini, umesema jimbo la Mbeya mjini linahitaji viongozi wenye maono na uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi kama ilivyo sasa chini ya Mbunge wake Dkt. Tulia Ackson Mwansasu.


Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa umoja huo Clemence Mwandemba wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Kalobe jijini humo.


Amesema Serikali ya awamu ya sita haina mfano kwani imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara za jiji la Mbeya, mpango wa kujengwa kwa kituo kikubwa cha mabasi jijini humo, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya na uboreshaji miundombinu ya elimu jijini Mbeya.


Kutokana na utendaji huo anaosema unaridhisha, amewataka wananchi kwenda kuwachagua viongozi wa mitaa kutoka Chama Cha Mapinduzi kwenye uchaguzi wa baadaye mwaka huu.


"Jiji la Mbeya tunasema tumetulia na Dkt. Tulia Ackson (Mbunge Mbeya mjini) na tunasema tumetulia na Dkt. Samia (Rais wa Tanzania) na tunatamba nao kwasababu kazi zenyewe mnaziona hata hapa Kalobe barabara yetu hii sio siku nyingi kitu cheusi kinatandikwa (Lami), jiji la Mbeya linahitaji viongozi wenye akili. Vijana wenzangu tuhakikishe tunajitokeza kujiandikisha kwenye daftari la mkazi nje la vile vichinjio (kadi ya mpiga kura) lazima tujiandikishe na tutawaletea wagombea wazuri CCM", ameeleza Mwandemba.



Diwani wa kata ya Kalobe Mhe. Ally Yassin ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ambapo amesema kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa hana mashaka na ushindi wa CCM.


Naye Diwani wa kata ya Mwakibete Mhe. Lukas Mwampiki amesikika akisema CHADEMA ni genge la kujipatia madaraka kwa njia nyepesi na kwamba Chama chake hicho cha zamani kimegawanyika kwakuwa ni mali  ya mtu hivyo kuwataka wananchi kuendelea kuiamini CCM.


Katika mkutano huo wa jumuiya ya vijana wa CCM Mbeya mjini wanachama kadhaa kutoka upinzani hasa CHADEMA wamepokelewa kuwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM).


Haya ni maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa ambapo UVCCM inaendelea kueleza miradi iliyotekelezwa na iliyo mbioni kutekelezwa huku pia wakitumia mikutano hiyo kuhimiza wanachama na wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuchagua viongozi bora kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji Novemba 27, 2024.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI