Na, Matukio Daima App,
Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wa ACT Wazalendo, wamewataka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillius Wambura Kuachia nafasi zao kutokana na mfululizo wa matukio ya utekaji na kuuawa kwa wananchi kuendelea kuongezea nchini huku wanaofanya matukio hayo kutokamatwa.
Viongozi hao wamesema hayo leo Jumatatu Septemba 9, 2024 mkoani Tanga, wakati wakitoa salamu, kwenye msiba wa aliyekuwa kada wa Chadema, Ali Kibao aliyezikwa leo.
Kibao, aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema alichukuliwa jioni ya Septemba 6, 2024 eneo ya Kibo Complex Tegeta jijini Dar es Salaam na watu wasiojulikana, akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga na basi la Tashriff na mwili wake kupatikana jana Jumapili Septemba 8, 2024 eneo la Ununio, Dar es Salaam.
Akitoa Salamu za pole, Godbless Lema, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, amemtaka, Waziri Masauni kutokwenda kwenye misiba ya watu waliotekwa tena kwani nilitarajia toka jana ungejiuzulu nafasi yako.
“Mheshimiwa Waziri nikuombe sana usiende tena kwenye msiba wa mtu aliyetekwa, nenda kwenye msiba wa mtu ambaye ameuawa. Mnatuumiza, nilitarajia baada ya statement ya Rais jana, wewe leo uwe umejiuzulu, IGP amejiuzulu na viongozi wengine wakae kando.
“Sisemi mambo haya kukuvunjia heshima, lakini wewe ni Waziri wa Mambo ya Ndani tusaidie, najiuliza hata nikiwa na kosa polisi wakija kunikamata natokaje,” amesema Lema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti (Bara) wa ACT Wazalendo, Isihaka Machinjita amesema: “Tukio lililotukutanisha hapa ni la ndugu yetu (Ali Kibao) ambaye ameuawa, tukio la namna hii linazusha hofu juu ya usalama wetu, tuna swali juu ya usalama wetu, ndugu yetu huyu ameuawa kwa sababu Jeshi la Polisi limeshindwa kulinda usalama wa raia na mimi niunge mkono alichosema Lema.
“Wakati mimi nipokuwa naangalia kwenye mtandao unakuja (Waziri Masauni), nikasema sisi tulishatoa wito kwamba mheshimiwa waziri angechukua hatua za kujiuzuru tangu matukio haya yalipotokea,” amesema Machinjita.
0 Comments