Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
OFISI ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeeleza kuwa si sahihi Kwa wadau ambao wamekuwa wakitumia majibu ya uchunguzi yanayotolewa na ofisi hiyo kwa kuwaeleza wananchi kwamba dawa fulani inatibu ugonjwa kwa lengo la kuvutia wateja.
Hayo yamemwa na Mkemia Mwandamizi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Ramadhani Nauja katika mahojiano kwenye maonesho ya Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yanayofanyika mjini Singida.
Alisema kitu anachokifanya Mkemia Mkuu wa Serikali si kuthibitisha kwamba dawa hii inatibu ugonjwa fulani bali ni kuhakikisha ubora wa dawa hiyo kwamba haina madhara kwa mtumiaji.
"Kuthibitisha kwamba hiyo dawa inatibu kweli au laa hilo sio jukumu la Mkemia Mkuu wa Serikali, bali jukumu la mamlaka ni kuangalia ubora wa bidhaa husika kwa afya ya watumiaji," alisema.
Aidha, aliwashauri wadau hao kuacha kutumia majibu ya uchunguzi unaofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali kuieleza jamii kuwa dawa hiyo imethibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali kuweza kutibu
Aliongeza kuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye mitambo ya kisasa ili kwenda na kasi ya teknolojia na kuharakisha utoaji wa haki nchini.
"Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imepata ithibati ya ubora wa kimataifa hivyo matokeo ya uchunguzi katika Maabara hii yanatambulika kimataifa," alisema.
Kuhusu maabara ya uchunguzi wa vinasaba vya binadamu, alisema m huduma hiyo imekuwa ikisaidia jamii katika uchunguzi wa kujua uhalali wa wazazi kwa mtoto, kutatua changamoto ya kujua mahusiano ya kindugu katika masuala ya mirathi.
Alisema pia DNA imekuwa ikisaidia katika masuala ya kitabibu mfano wanaotaka kupandikizwa figo au uroto lazima wote hao waweze kupima na kujua mahusiano ili viungo vinavyopandikizwa katika miili yao visilete madhara kwa yule anayewekewa.
"Maabara ya vinasaba vya binadamu inatusaidia kubaini masuala ya jinai kwa watu wanaoshiriki matukio ya uharifu,wizi,unyang'anyi,ujambazi ,hawa wote huwa tunawafanyia uchunguzi," alisema.
0 Comments