NA WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni ameongoza Wananchi wa Kijiji cha Ruvu Mbuyuni Kata ya Mabilioni katika harambee ya kuchangia uibuaji ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho kuondoa adha wanayokabiliana nayo ya kulazimika kutembea umbali wa Kilomita 25 kutoka kijijini hapo hadi Kituo cha Afya Hedaru kilichopo Kata ya Hedaru kufuata huduma za Afya.
Wakizungumza kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika Kijijini hapo wa kusikiliza na kutatua kero na malalamiko ya Wananchi, baadhi yao wamesema zipo changamoto nyingine ambazo wanakabiliana nazo kwenye Kijiji chao ikiwemo kukosa miundombinu mizuri ya barabara, maji safi na umeme.
Lakini suala la kukosa Zahanati kwao limekuwa changamoto kubwa sana ambalo linahitaji ufumbuzi wa haraka kwani yapo matukio ya kuwapoteza wapendwa wao, lakini pia mama waja wazito kujifungua wakiwa njiani kuelekea Kituo cha Afya hedaru kupata msaada wa matibabu.
Aidha kufuatia kwa hali hiyo, Kasilda alilazimika kuongoza harambee hiyo na kufanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi Milioni 4.3 pamoja na vifaa vya ujenzi ikiwa ni pamoja na Saruji, Mchanga, Mabati, na Maji.
“Kutoka Ruvu Mbuyuni hadi Hedaru kilometa 25 ni mbali sana, kwenye hili lazima tuwe kitu kimoja jamani wakati Serikali inaendelea na mpango wake mimi naomba kama eneo lipo tuanze msaragambo haraka (nguvu kazi) Serikali itakuja kumalizia" Alisema Kasilda.
Na kuongeza "Na kwenye hili lazima tufanye harambee hapa tuweze kuanza ujenzi wa zahanati haraka, lakini ili kuonesha kuwa hili jambo limeniingia leo hapa lazima tuchangie, tutakuja kufanya harambee lakini harambee ya kwanza tunaifanya leo hapa kwahiyo kila aliyekuja hapa lazima achangie na kutoa ahadi hapa tunaongelea suala la uhai hapa”.
Kwa upande wake Katibu Mwenezi Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same, Mohamed Ifanda amesema baadhi ya Wakazi wa Kijiji hicho wamekuwa wakilazimika kuishi maisha ya namna mbili ambapo mtu akiwa na familia na mke mjamzito analazimika kumpangishia nyumba Hedaru ili aweze kuwa karibu na huduma za Afya na kuweza kuhudhuria hatua zote ambazo mama mjamzito anapaswa ili aweze kujifungua salama.
Pia kuhusu suala la Maji kwa mujibu wake Meneja wa Wakala wa usambazaji maji na usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Same, Mhandisi Abdallah Gendaeka amesema kuwa tayari hadi kufikia Septemba 25 mwaka huu 2024 gari la kuchimbi kisima litakuwa limefika kijijini hapo kuanza utekelezaji.
Suala la Umeme nalo Shirika la Umeme nchini (TANESCO) tayari limeanza kuweka nguzo na kazi inaendelea kuhakikisha umeme kijijini hapo unawake,
Kwa upande wa barabara Meneja wa Wakala wa barabara za mijini na Vijijini (TARURA) Same, Mhandisi James Mnene amesema ameshafanya hatua za awali kwa kutembelea na kuangalia hali ya barabara hiyo kwa ajili ya maandalizi ya bajeti na sasa kipaumbele chao ni katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2025/26 kutenga fedha kuifungua barabara hiyo.
Mwisho.
0 Comments