Header Ads Widget

CHADEMA MBARALI WATUMIA MICHEZO KUHIMIZA USHIRIKI SERIKALI ZA MITAA.

 



NA JOSEA SINKALA, MBEYA.


Aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Mbarali ambaye pia ni mtia nia ya ubunge jimboni humo Liberatus Mwang'ombe (CHADEMA), ameendesha ligi katika kata zote za jimbo la Mbarali kwa lengo la kuhimiza wananchi kujiandikisha kwenye daftari la mkazi na daftari la wapiga kura wakati utakapowadia na kuchagua viongozi bora kwa maendeleo yao.


Ligi hiyo imefanyika katika viwanja mbalimbali vya jimbo la Mbarali ambapo ufunguzi na fainali vilishuhudiwa katika uwanja wa lembuka ya zamani jirani na Polisi Chimala wilayani humo.


Akizungumza kwenye kilele cha ligi hiyo, mfadhili wa ligi hiyo Liberatus Mwang'ombe ambaye ni mtia nia ya ubunge jimbo la Mbarali kwenye uchaguzi mkuu ujao, amesema kubwa zaidi ni kuibua vipaji, kujenga afya, kuimarisha upendo na kujenga urafiki pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji.


"Tumefanya mashindano yetu kwa malengo, malengo yetu mwaka huu lengo letu kuu ni kuhamasisha kila mtu kujiandikisha kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa hakikisheni mnajitokeza", ameeleza Mwang'ombe.



Kwa upande wake mgeni rasmi aliyefunga ligi hiyo ya Mwang'ombe Cup 2024 Frank Mwakajoka ambaye ni Makamu mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya Nyasa, amewataka wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la mkazi na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la wapiga kura ili kupata haki ya kushiriki kuchagua viongozi wanaowataka.


Mwakajoka amempongeza muandaaji wa michuano hiyo Liberatus Mwang'ombe kwa kuwakusanya pamoja wananchi  bila kujali tofauti zao za kisiasa na kidini ili kujenga undugu na kuboresha afya zao kupitia michezo.



Shughuli hiyo imehudhuriwa na maelfu ya wananchi na wanachama wa Chadema kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo la Mbarali na viongozi mbalimbali wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Njombe Rose John Mayemba, aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyasa na aliyekuwa Katibu wa CHADEMA mkoa wa Mbeya mwalimu Titho George.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI