NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
HATIMAYE Wananchi wa kata ya Makuyuni wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wanaenda kuondokana na changamoto ya ubovu wa barabara ya Himo - Makuyuni - Lotima baada ya serikali kutoa Bilioni 3.681 kwa ajili ya barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya barabara hiyo kwa Mkandarasi kampuni ya Kings Building, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga katika soko la Himo, alisema kuwa, kujengwa kwa barabara hiyo kutasaidia kuinua uchumi wa kata ya Makuyuni.
Alisema kuwa, barabara hiyo ilikuwa kero kubwa kwa wananchi hivyo serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuonyesha dhamira yake kwa vitendo ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
"Mwaka 2020 wakati tukiwanadi wagombea wa ccm ambao ni Rais, Mbunge na Diwani tuliwaahidi wananchi mkiwachagua viongozi wanaotokana na chama chetu barabara hii tutaijenga na sasa tumekuja kutekeleza ahadi yetu kwa vitendo" Alisema Naibu Waziri Ummy.
Alimshukuru sana Rais Dkt Samia kwa kutoa fedha Bilioni 3.6 kujenga Barabara hiyo ambayo imekua kero kubwa kwa wananchi hao kwa miaka mingi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Dkt. Charles Kimei alisema kuwa, alimtaka Mkandarasi kushirikiana na viongozi wa kata na vitongoji ili waweze kuwaelezea jografia ya eneo inapopita barabara hiyo ili waweze kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha mradi huo unadumu.
Dkt. Kimei alitumia nafasi kumtaka pia Mkandarasi huyo kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unazingatia thamani ya fedha kwani barabara hiyo ni ya kimkakati ambapo inaunganisha wilaya ya Moshi na wilaya ya Mwanga.
Naye Mbunge wa Viti maalum kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Shally Raymond alisema kuwa, barabara hiyo imekuwa ikipambaniwa muda mrefu sasa lakini sasa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeamua kuijenga kwa kiwango cha lami.
Mbunge Shally alisema kuwa, barabara hiyo ni mwarobaini wa kupunguza foleni katika barabara kuu ya Himo kwenda Dar es salaam pamoja na kupunguza ajali.
"Nikuombe Mkandarasi uipe kipaombele barabara hii na uzingatie uimara wa barabara ili iweze kudumu muda mrefu na niwaombe wananchi wa kata ya Makuyuni toeni ushirikiano kwa Mkandarasi ikiwa ni pamoja na kulinda vifaa vitakavyoletwa kwa ajili ya barabara hii" Alisema Mbunge Shally.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (TARURA), Mhandisi Nicolaus Francis alisema kuwa, serikali imetoa Bilioni 3.681 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kilomita 6.115.
Mhandisi Francis alisema kuwa, ujenzi wa barabara hiyo ni miezi sita ambapo lengo lake ni kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara na wananchi wanaofanya shughuli za kibiashara na kilimo kuzunguka eneo la kata ya Makuyuni na kuimarisha huduma za usafiri kwa wananchi kwenda kupata huduma za Elimu, Afya na mahitaji mbalimbali katika mji wa Himo.
"Ujenzi wake utahusisha ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua, ujenzi wa vivuko vya kwenye makazi na ujenzi wa makalavati pamoja na kuweka taa za barabarani baadhi ya maeneo" Alisema Mhandisi Francis.
Mwisho..
0 Comments