Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Treni ya abiria ya Shirika la reli nchini (TRC) iliyokuwa ikisafiri kutoka mkoani Kigoma kuelekea Dar es Salaam imeanguka katika wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma usiku wa kuamkia leo Agisti 28 ambapo watu 70 waliokuwa kwenye treni hiyo wamejeruhiwa.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Filemon Makungu amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo iliyotokea kati ya stesheni ya Lugufu na Uvinza wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma majira ya saa nane usiku kuamkia Agosti 28.
Akieleza kuhusu hali ya majeruhi Kamanda huyo wa polisi mkoa Kigoma alisema kuwa watu 61 ndiyo waliopata majeruhi ambapo kati yao 15 wameumia Zaidi huku abiria watano wakielezwa kuumia vibaya kuhitaji msaada wa matibabu makubwa Zaidi.
Baada ya ajali hiyo Abiria waliwahishwa kituo cha afya Uvinza wilayani Uvinza kwa ajili ya matibabu ambapo jitihada zilifanywa usiku huo kuhakikisha abiria watano waliokuwa wameumia Zaidi wanahamishiwa hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma Maweni.
Mabehewa sita ya abiria yaliyokuwa nyuma ndiyo yaliyoanguka sambamba na behewa la mizigo na breki.
Akitoa taarifa kwa niaba ya Mkuu wa mkoa Kigoma, Thobias Andengeye Mkuu wa wilaya Kigoma, Salum Kali alisema kuwa hakuna vifo wala madhara makubwa yaliyojitokeza kwenye ajali hiyo na kwamba majeruhi wote walipatiwa matibabu ya haraka.
Pamoja na hilo Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa baada ya ajali hiyo taratibu zilifanywa na treni kuendelea na safari majira ya alfajiri kuamkia jana ambapo abiria waliokuwa kwenye mabehewa yaliyoanguka walihamishiwa kwenye mabehewa mengine.
Kali alisema kuwa tayari shirika la reli limeanza uchunguzi kujua sababu hasa zilizosababisha ajali hiyo huku taratibu nyingine kwa ajili ya abiria na majeruhi zikiendelea.
Mwisho.
0 Comments