Wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Kanda ya Mashariki na Pwani takribani 70 wamelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wote ambao wanadaiwa kuhusika na unyanyasaji wa Binti mmoja mkazi wa Yombo Dovya Temeke jijini Dar es Salaam .
Katika tamko la pamoja ambalo wamelitoa August 7, 2024, wametoa wito kwa Jeshi hilo kuhakikisha kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha Mahakamani mapema iwezekanavyo, ambapo wamedai kuwa upelelezi wa tukio hilo sio wa kuchukua muda mrefu kwa kuwa kuna vithibitisho ambavyo vinaweza kutumika kuwabaini haraka.
Tamko hilo ambalo limesomwa limetolewa kwa pamoja na takiribani wanachama 70, kutoka mikoa ya Dar es salaam, Pwani na Morogoro wamesema kuwa wanasikitishwa na kitendo hicho huku wakitaka pia mtuhumiwa anayetajwa kama bosi (afande) naye akamatwe kwa ajili ya hatua za kisheria.
"Sisi watetezi wa haki za binadamu Nchini tumesikitishwa sana na ukatili huo na tunataka wahusika wote akiwemo huyo bosi wao (Afande) wakamatwe na kufikishwa Mahakamani kwa mujibu wa Sheria za Nchi yetu" amesema
Wamesisitiza kuwa Ibara ya 12 na 13 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinalinda heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa Utu wa Mtu na kupinga ubaguzi wa aina yoyote hile.
Wameeleza kuwa nchini ipo Kanuni ya Adhabu ambayo katika kufungu cha 131 A(1) (2) kinatoa adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa Mtu au Watu wakithibitika kufanya ubakaji wa kundi (gang rape), kama inavyodaiwa kutokea kwa binti huyo maeneo ya Yombo Dovya Temeke.
Wameongeza kuwa kwa kuwa Binti huyo alionekana kulawitiwa wamedai kuwa pia kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha 154 (1) cha kanuni ya Adhabu na kuwa kifungo chake ni maisha jela au miaka 30. Lakini pia wamedai kuwa kitendo cha kusambaza video ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Aidha wadau hao wametoa wito kwa jamii kutosambaza zozote kuhusu tukio hilo ambazo ni kinyume na Sheria ya Makosa ya kimtandao na Sheria ya kulinda taarifa binafsi.
Tamko hilo limesainiwa na Mratibu wa wa Kanda, Michael Marwa, ambapo Mratibu huyo amesema kuwa wito wao mwingine wanauekekeza kwa Rais Samia ambapo wameshauri kutumia mamlaka yake kuunda chombo huru ambacho kitakuwa kikichunguza matukio yote ambayo yatajwa kuhusishwa na baadhi ya watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama.
0 Comments