Mkuu wa TAKUKURU mkoa Kigoma Stephen Mafipa akiwa katika mkutano na waandishi wa habari akitoa taarifa ya utendaji ya Taaaisi hiyo kwa kipindi cha mwezi April hadi Juni mwaka huu
*******************
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Kuchelewa kutumika kwa vifaa vya ujenzi wa miradi ya maji katika halmashauri ya wilaya Uvinza mkoani Kigoma kunaelezwa kuitia hasara serikali kutokana na vifaa hivyo kukaa muda mrefu na kuharibika hivyo mradi unapoanza kutekelezwa inabidi vifaa vingine vinunuliwe.
Hayo yamebainishwa na Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa Kigoma katika taarifa ya utendaji na utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika kipindi cha April hadi Juni mwaka huu.
Mkuu wa TAKUKURU mkoa Kigoma, Stephen Mafipa alisema hayo akitoa taarifa mbele ya waandishi wa Habari ofisini kwake mjini Kigoma ambapo alisema kuwa kuchelewa kutekelezwa kwa wakati kwa miradi mingi ya maji kunaitia hasara serikali.
Mafipa alisema kuwa moja ya changamoto kubwa inayojitokeza ni kununuliwa mapema kwa vifaa vya miradi na kupelekwa maeneo ya utekelezaji lakini vifaa hivyo havitumiki kwa wakati na kukaa muda mrefu eneo la mradi huku mradi ukiwa umesimama na hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kunusuru kuharibika kwa vifaa hivyo.
Kutokana na hilo TAKUKURU mkoa Kigoma imeshauri serikali na halmashauri kununua na kupeleka vifaa eneo la mradi wakati mradi unaanza kutekelezwa au vifaa vilivyopo eneo la mradi viazimwe kwenye mradi mwingine na kurudishwa mradi utakapokuwa unataka kuanza tena.
Katika hatua nyingine TAKUKURU imesema kuwa kutokuwepo kwa nyenzo za tathmini ya msamaha kwenye utoaji huduma za afya wilaya ya Buhigwe kumefanya huduma za matibabu katika wilaya hiyo kuwa kubwa na kulalamikiwa na wagonjwa wanaoenda kupata matababu kwenye vituo vya afya vya serikali.
Kutokana na hali hiyo Mafipa alisema kuwa uchunguzi wa TAKUKURU umebaini baadhi ya watoa huduma kwenye vituo vya afya vya serikali kuwashawishi wagonjwa kwa kuchukua mawasiliano yao na kuwatoa kupata huduma kwenye taasisi za utoaji huduma za serikali na kuwapeleka vituo binafsi.
Mkuu wa TAKUKURU mkoa Kigoma,Stephen Mafipa alisema kuwa hali hiyo inaikosesha serikali mapato na hivyo kushauri kuandaliwa kwa nyenzo ya tathmini ya msamaha kwa mujibu wa sera ya matibabu ya mwaka 2017 ili kuwezesha tathmini ya msamaha kufanyika.
0 Comments