Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
matukiodaima3@gmail.com
KATIBU Tawala Mkoa wa Singida, Dk.Fatuma Mganga, amewataka Maafisa Mipango na Maafisa Lishe katika mikoa ya kanda ya kati kuonesha uzalendo katika kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto kwa kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya masuala ya lishe zinaelekezwa huko na sio kulipana posho.
Alisema hayo juzi wakati akifungua semina ya utoaji wa matokeo ya utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria ambao ulifanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Semina hiyo imewashirikisha Maafisa Mipango,Wauguzi, Waratibu wa Malaria,Mameneja Takwimu,Maafisa Lishe,Waganga Wakuu wa Wilaya na waratibu wa huduma za mama na mtoto kutoka mikoa ya Dodoma,Singida na Manyara.
Dk.Mganga alisema tatizo la udumavu katika mikoa ya kanda ya Kati ni kubwa sana na limefikia asilimia 28.9 kwasababu fedha zinazotengwa kwa ajili ya masuala ya lishe inawezekana zinatumika kulipana posho badala ya kukwamua changamoto hiyo.
"Matokeo yanaonyesha hali ya udumavu bado ni kubwa ambapo ni asilimia 28.9,takwimu hii ni karibu sawa na wastani wa kitaifa ambao ni asilimia 30,hali hii imesababisha kuendelea kuwepo kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano," alisema.
Dk.Mganga alitoa mchanganuo kuwa Mkoa wa Manyara ndio unaoongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha udumavu ambacho ni asilimia 32, ikifuatiwa na Dodoma yenye asilimia 30.7 na Mkoa wa Singida una asilimia 25.7.
Alisema inashangaza kuona mikoa ya kanda ya kati masuala ya kutenga fedha kwa ajili ya lishe inafanya vizuri lakini tatizo la udumavu inakuwa vinara hali ambayo inaonesha fedha hizo haziakisi uhalisia ambao unatakiwa.
"Yawezekana unapanga fedha za lishe lakini mwanzo mwisho umepanga ya kikao,hela ya kusaidia watoto tunajisaidia sisi wenyewe,masuala ya posho tugawane kwenye vyanzo vingine lakini za lishe tuache ili angalau tusaidie masuala ya lishe," alisema.
Dk.Mganga alisema kimsingi suala la udumavu katika mikoa ya kanda ya kati halisababishwi na wazazi bali linasababishwa na watalaam ambao wameshindwa kuwajibika vyema katika majukum waliyopewa na kwamba wakati sasa umefika kubadilika ili kuondokana na tatizo la udumavu kwenye mikoa hiyo.
Naye Meneja Takwimu Mkoa wa Singida, Naing'oya Kipuyo,ambaye alimwakilisha Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk.Albina Chuwa katika semina hiyo alisema utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria wa mwaka 2022 ulifanywa bmna Ofisi ya Taifa ya Takwimu na ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.
Alisema malengo ya utafiti huo ni kuangalia taarifa za sasa za viashiria vya afya ya uzazi na mtoto na malaria kama vile takwimu zinazohusu hali ya makazi,ndoa,kiwango cha uzazi,afya na lishe,uzazi wa mpango,afya ya uzazi,upendeleo wa kizaa.
Kipuyo alisema utafiti huo pia ulikuwa unaangalia huduma kwa wajawazito,vifo vya watoto,vifo vinavyotokana na uzazi,afya za watoto,lishe kwa watoto na watu wazima,malaria,chanjo kwa watoto,unyanyasaji wanawake majumbani,ukeketaji na masuala mengine ya afya.
Naye Mtakwimu Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dodoma, Prisca Mkongwe, alisema katika utafiti walioufanyika 2021/2022 hali ya udumavu kitaifa ni asilimia 30 na suala la vifo vya akina mama wajawazito vimepungua kutoka 503 na kufikia 104 katika kila vizazi hai 100,000.
Mkongwe alisema katika kipindi cha 2015/2016 asilimia 63 ya watoto walikuwa wanafariki kabla ya kufikisha miaka mitano lakini hivi sasa kiwango hicho kimepungua na kufikia asilia 43 katika kila vizazi hai 100,000.
Naye Afisa Lishe wa Mkoa wa Singida, Teda Sinde, alisema kiwango cha udumavu katika mkoa huo kimepungua kutoka asilimia 29 na kufikia asilimia 25 hii ni kutokana na jitihada zinazofanyika katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya lishe.
Sinde alisema changamoto ya udumavu inasababisha na ulishaji na unyonyeshaji watoto wadogo hivyo kutokana na hali hiyo mkoa umejipanga inaanzisha mapishi darasa katika vijiji ili kuwapa elimu ya lishe wananchi.
MWISHO
0 Comments