Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Njombe Christopher Sanga ameagizwa kuhakikisha anaanza haraka kazi ya ukusanyaji mapato katika vyanzo vipya ambavyo havikufanikiwa kukusanywa katika mwaka uliopita vikiwemo vya Kokoto na Ardhi ili kupandisha makusanyo.
Katika mkutano wa baraza la madiwani mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya ya Njombe Mhe.Valentino Hongoli amesema Hadi wanamaliza mwaka wa fedha ulioisha mwezi Juni mwaka huu Halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya mapato kwa 86% huku jitihada zaidi zikitakiwa kuongezwa kwa wakusanyaji.
Aidha Mhe.Hongoli amesema kutokana na hali hiyo ni lazima Mkurugenzi aanze kuchukua hatua haraka za kukusanya mapato hayo hasa kwenye vyanzo hivyo vipya ambavyo katika mwaka uliopita havikukusanywa na hii itachagiza kupanda kwa makusanyo.
Naye mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Njombe Mhe.Justin Nusulupila amesema ni lazima kuwepo na mshikamano wa wataalamu wote pamoja na Chama katika kuhakikisha maendeleo yanasonga mbele ili kufikisha azma ya serikali ya kuwahudumia wananchi.
Kutokana na mapato mengi katika halmashauri hiyo kutegemea zaidi mazao ya misitu baadhi ya madiwani akiwemo Mhe.Javan Ngumbuke wametaka kuwekwa msisitizo wa upandaji miti kwa kuwa viwanda vidogo vidogo vya wachina vya kuchakata mazao hayo vimekuwa vikiongezeka.
Wengine akiwemo Mhe.Getrude Chungwa na Mhe.Innocent Gwivaha wametaka kuendelea kuboreshwa kwa huduma za afya kwenye Zahanati na Hospitali ya wilaya ili kuwanusuru wagonjwa.
0 Comments