NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Mwenge wa uhuru mwaka 2024 umeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji wa Itagano Mwasenkwa jijini Mbeya na kuwataka wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji kwa faida yao wenyewe.
Akizungumza kwenye zoezi la ukimbizaji mwenge wa uhuru, kiongozi wa mbio za mwenge mwaka huu Godfrey Mzava, ameipongeza mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mbeya kwa kujenga mradi huo kwa mapato ya ndani ili kuendelea kutatua kero ya upatikanaji wa maji kwa wananchi jijini Mbeya kutokana na ongezeko la watu kila uchao.
"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan shauku yake ni kuona huduma ya maji ambayo ni huduma muhimu sana na haina mbadala inasogezwa kwa wananchi, ninaweka jiwe la msingi mradi huu lakini zingatieni maelekezo yote tuliyokubaliana baada ya kupitia nyaraka zote hapa", ameeleza Mzava na kuongeza kuwa;
"Niwaombe wananchi tuwe watunzaji wa miradi hii hasa shughuli mnazofanya msifanye hadi kwenye vyanzo vya maji", amesisitiza kiongozi huyo wa mbio za mwenge mwaka 2024.
Akitoa taarifa ya mradi wa maji maji Itagano Mwasenkwa, Mhandisi Barnabas Konga kutoka mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mbeya, amesema mradi huo utawanufaisha maelfu ya wananchi wa kata za Mwasenkwa, Ilemi na Iganzo jijini humo hasa ambao walikuwa hawapati huduma ya maji safi na tayari mradi huo ulishaanza kutoa maji kwa wananchi na mpaka sasa umefikia asilimia 82 ukitarajiwa kukamilika Desemba 2024 kwa gharama ya shilingi Billion 5.2.
Kwa upande wake Mbunge wa viti maalum mkoa wa Mbeya Suma Fyandomo, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kutoka vyanzo mbalimbali ili kutekeleza miradi kwa manufaa ya wananchi.
Diwani wa kata ya Mwasenkwa Juma Changani, amesema mradi huo utaleta tija zaidi kwa wananchi wake pamoja na kata jirani za Ilemi na Iganzo huku mstahiki meya wa jiji la Mbeya Dour Mohamed Issa akimshukuru pia Mbunge wa Mbeya mjini Dkt. Tulia Ackson kwa kuendelea kupigania haki na maslahi ya wananchi wake.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na kituo hiki baada ya kuwekwa jiwe la msingi wamesema watanufaika na mradi wa maji Itagano Mwasenkwa kwani awali walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma lakini kwa kipindi cha hivi karibuni tayari wameanza kupata huduma ya maji kutoka kwenye mradi huo.
Mwenge wa uhuru umeweka jiwe la msingi mradi wa maji Itagano Mwasenkwa kwenye eneo la Mwasenkwa palipojengwa mtambo mkubwa wa kuchuja na kusambaza maji kwa wananchi ambapo kiongozi wa mbio za mwenge mwaka 2024 amepongeza juhudi za mamlaka ya maji Mbeya kuwahudumia wananchi na kuwaasa kuzingatia maelekezo yake ili kuona fedha za umma zinaendana na thamani ya miradi katika kuchochea maendeleo endelevu na kuleta ustawi wa jamii.
0 Comments