Na Gabriel Kilamlya Matukio DaimaAPP NJOMBE
Wakati Bunge likifanya marekebisho ya sheria mbalimbali za Kodi,Mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa Njombe imetakiwa kutumia mbinu mbalimbali kuwafikishia elimu hiyo wafanyabiashara ili waweze kuelewa na kuchukua hatua ya kulipa kodi kwa hiari.
Mkuu wa mkoa wa Njombe Antony Mtaka anatoa kauli hiyo baada ya Maofisa wa Kodi toka TRA Makao makuu kufika na kutoa elimu ya mabadiliko ya sheria mbalimbali zikiwemo zile zinazohusisha misamaha ya kodi ya Ongezeko la Thamani VAT Kwenye baadhi ya bidhaa yakiwemo magari yanayotumika katika ujenzi wa barabara.
Ofisa msimamizi mkuu wa kodi toka TRA Makao makuu Lameck Ndinda anasema baada ya mabadiliko ya sheria hizo wamelazimika kuanza kutoa elimu kwa nchi nzima juu ya utekelezaji wake huku wafanyabiashara wakitakiwa kuzifuatilia kwa karibu na kuzifanyia kazi.
Naye kaimu meneja wa TRA Mkoa wa Njombe Beatrice Kahoho anaendelea kuomba ushirikiano wa dhati toka kwa wafanyabiashara hao ili kufanikisha lengo la serikali la kukusanya kodi kwa maendeleo ya Taifa.
Tumain Haule na Lustin Kyando ni baadhi ya wafanyabiashara mkoani Njombe ambao licha ya mabadiliko ya sheria hizo za kodi lakini bado wanaiomba serikali kuona uwezekano wa kuwapunguzia kodi kwani bado ni mzigo mkubwa.
Wengine wanakiri kuelimishwa juu ya sheria hizo lakini wanataka elimu hiyo kwa upana zaidi.
Katika mwaka mpya wa fedha wa 2024/2025 TRA Mkoa wa Njombe wamepangiwa kukusanya shilingi bilioni 35 ambazo zinahitaji jitihada za pamoja kati ya wafanyabiashara na Mamlaka hiyo.
0 Comments