Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima App,Dodoma
WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde ametoa zuio kwa raia wote wa kigeni kuingia kwenye leseni za uchimbaji mdogo (PML)bila kufuata taratibu zilizoelezwa kwenye Kifungu cha 8 cha Sheria ya Madini Sura ya 123.
Zuio hilo amelitoa jijini Dodoma alipotembelea eneo lenye mgogoro kati ya mwenye leseni na wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Handali Wilayani Chamwino-Dodoma kufuatia malalamiko ya raia ya kigeni kuingia kwenye Leseni ndogo ya uchimbaji na kujeruhi mchimbaji mdogo.
"Dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona nchi inaongeza uwekezaji lakini unaofuata taratibu na pia kwa upande wa pili kuona wachimbaji wadogo wananufaika na rasilimali madini kupitia shughuli za uchimbaji.
"Leseni za uchimbaji mdogo ni kwa ajili ya Watanzania, hivyo sitaraji kuona Raia wa Kigeni anaingia kwenye leseni hizo pasipo makubaliano maalum ya msaada wa kiufundi ambayo yamesajiliwa na Tume ya Madini.
Kutokana na migogoro mingi inayojitokeza baina ya mwenye leseni na wachimbaji wadogo wenye maduara, zimeandaliwa Kanuni ambazo zimeweka masharti kwa mmiliki wa leseni kuzuia wachimbaji wadogo kuchimba ndani ya Leseni yake au ikiwa ametoa ridhaa basi ni sharti ni kuingia mkataba na wote wanaochimba katika leseni yake ili kulinda maslahi yao na kuwaelekeza maafisa madini nchi nzima kufanya operesheni ya ukaguzi wa mikataba ya msaada wa kiufundi.
Pia naagiza Afisa Madini wote nchini kuhakikisha wamiliki wote wa leseni za kubwa za Biashara ya madini(Dealer Licence) hawaendi moja kwa moja kwa kwenye maeneo ya uchimbaji na badala yake waende kwenye masoko ya madini kama masharti ya leseni yao yanavyosema.
Kufuatia changamoto iliyojitokeza katika eneo hilo la mgodi na kupelekea madai ya mchimbaji mdogo kupigwa na raia wa kigeni ninavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua mara moja ili sheria ichukue mkondo wake”Alisema Mavunde
Awali, akieleza juu ya changamoto ya mgogoro huo, Katibu wa wachimbaji wadogo aliyefahamika kwa jina moja la Ndg.Nassoro Assenga alieleza kuwa wao kama wachimbaji wadogo hawana tatizo na uwekezaji unaofanywa na mmiliki wa Leseni, hitaji lao kubwa ni kukaa naye chini ili kuingia makubaliano ambayo yatakuwa yana manufaa kwa pande zote mbili.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule alimpongeza Waziri kwa kufika kutatua mgogoro huo na kuahidi kwamba atasimamia kupitia vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza ugomvi kati ya raia wa kigeni na mchimbaji na hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria
Mwisho
0 Comments