Header Ads Widget

WAZIRI MAVUNDE AKEMEA VITENDO VYA UDANGANYIFU KWENYE BIASHARA YA MADINI

Na Hamida Ramadhan Matukio Daima App Dodoma

WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde Amekemea vikali vitendo vya udanyanyifu kwenye biashara ya madini pamoja na utoroshaji wa madini vinavyofanywa na watu wachache ambao katika vitendo vyao, wanaturudisha nyuma katika malengo yetu. 


Hayo ameyasema leo Julai 28,2024 jijini  Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema Wizara itaendelea kuchukua hatua kali kwa wahusika wote watakaobainika wanajihusisha na utoroshaji wa madini.


Amesema Katazo la wageni kuingia kwenye PMLs bila TSA Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu ni muhimu katika kusimamia maendeleo na ustawi wa Sekta ya Madini. 


"Katika hili, Wizara itaendelea kusimamia Mfumo wa Kisheria na Usimamizi wa Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika kukiuka Sheria na Kanuni zinazosimamia Sekta hii," Amesema 


Na kuongeza "Wizara kwa kushirikiana na wadau itaendelea kufanya marekebisho ya Mfumo wa Kisheria na Usimamizi wa Sekta ya Madini pale itakapoonekana kuna umuhimu ili kuendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika Sekta hii muhimu kwa uchumi wa nchi, " Amesema


Katika hatua nyongine Waziri Mavunde amesema Kumetokea tabia ya wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini kuingia makubaliano yasiyo rasmi na wageni kutoka nje ya nchi na kuwaruhusu kufanya kazi katika leseni zao. Ikumbukwe kwamba, leseni za uchimbaji mdogo wa madini zinatolewa kwa Watanzania pekee kwa mujibu wa Kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Madini, Sura 123.


Amesema Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Madini, Sura 123 kimeweka wazi kwamba, kwa mmiliki wa leseni ndogo ya uchimbaji wa madini, pale atakapohitaji msaada wa kiufundi ambao haupatikani nchini, anaruhusiwa kuingia makubaliano na mgeni kutoka nje ya nchi kupata huduma hiyo baada ya makubaliano hayo kupitishwa na Tume ya Madini.


Ameeleza kuwa,Athari kubwa zinazotokana na kutozingatiwa kwa kifungu cha 8(3) ni pamoja na; wachimbaji wengi wadogo waliokuwa wakiendelea na shughuli zao za uchimbaji katika leseni husika huathirika kwa kukosa ajira, kupoteza mitaji yao waliyowekeza wakati wa uchimbaji pia huleta chuki kwa Serikali yao.


"Nachukua nafasi hii kupiga marufuku kwa wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini, kuingiza wageni kutoka nje ya nchi kwenye leseni zao bila kuwa na mikataba/makubaliano ya msaada wa kiufundi (Technical Support) yaliyopitishwa kwa mujibu wa Sheria, " Amesema Waziri Mavunde. 


Na kuongeza "Pia nichukue fursa hii kupiga marufuku wageni wenye leseni kubwa za biashara ya madini (dealer’s Licence) hususan wa madini ya vito kwenda machimboni kukusanya madini kwani Kufanya hivi ni kupora haki ya ajira ya Watanzania ambao kwa mujibu wa Sheria,kazi ya kufuata madini machimboni inapaswa kufanywa na Watanzania pekee wenye kumiliki leseni ya “broker”," Amesema .  

Amebainisha kuwa,Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini pamoja na wageni kutoka nje ya nchi watakaobainika  kukiuka matakwa ya Sheria.


"Naomba nitoe rai kwa wawekezaji wote wenye leseni za uwekezaji katika Sekta ya Madini kuzingatia matakwa ya Sheria ya Madini, Sura ya 123. Aidha, Wizara ya Madini itaendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji wote wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kufanya uwekezaji wenye tija na kukuza uchumi wa taifa letu kutokana na uvunaji wa rasilimali madini, "Amesema.


Hata hivyo amesema Mwenendo wa Makusanyo ya Maduhuli yatokanayo na Rasilimali Madini Katika kipindi cha Mwaka 2023/2024, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ilipanga kukusanya jumla ya Shilingi 882,121,205,000 kutokana na vyanzo vilivyoainishwa katika Sheria ya Madini Sura ya 123. 


Ameeleza vyanzo hivyo ni pamoja na Mrabaha, Ada ya Mwaka ya Leseni, Ada ya Ukaguzi wa Madini, Ada za Kijiolojia, Tozo ya Huduma ya Maabara na malipo ya adhabu mbalimbali. 


"Napenda kuwajulisha kuwa katika kipindi cha kuanzia Mwezi Julai, 2023 hadi tarehe 30 Juni, 2024, Tume ya Madini ilikusanya jumla ya Shilingi 753,815,646,587.13 sawa na asilimia 85.45 ya lengo la makusanyo lililopangwa, "Amesema Waziri Mavunde. 


Na kuongeza "Makusanyo haya ni sawa na ongezeko la kiasi cha Shilingi 76,080,867,802.38 ukilinganisha na fedha zilizokusanywa katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 ambapo makusanyo yalikuwa ni Shilingi 677,734,778,784.74 kwa lengo la kukusanya Shilingi 822,018,203,000.00," Amesema


Amesema Kuanzia Mwaka wa Fedha 2019/2020 hadi 2023/2024, makusanyo yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka na kutupa imani ya kufikia malengo ya kukusanya Shilingi 999,998,000,000.00 kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.


"Hapo nyuma kidogo, Wizara ilikuwa ikikusanya kiasi kidogo cha maduhuli ukilinganisha na sasa. Mathalan, Mwaka wa Fedha 2014/2015, Wizara ilikuwa na lengo la kukusanya Shilingi 209,957,882,999.00 na kufanikiwa kukusanya TZS 168,043,402,877.13," Amesema Waziri Mavunde. 


Aidha, Mwaka wa Fedha 2015/2016 lengo la makusanyo lilikuwa ni Shilingi 211,957,882,999.00 na kufanikiwa kukusanya Shilingi 207,917,127,854.55 ambapo ndani ya kipindi kifupi tunashuhudia ongezeko la makusanyo ya maduhuli yatokanayo na shughuli za uchimbaji wa madini. 


" Mabadiliko haya ni mafanikio makubwa ambayo wadau wote wa Sekta hii wanatakiwa kujivunia pia Mafanikio haya yanatokana na jitihada jumuishi za wadau mbalimbali kuanzia kwa wachimbaji wa madini wakubwa kwa wadogo, wafanyabiashara wa madini pamoja na Taasisi zote zinazohusika katika kuilea na kuisimamia Sekta ya Madini Nchini," Amesema 


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI