Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda ameitisha kikao cha dharura kati yake na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha (RPC) na Mkuu wa Upelelezi mkoa (RCO) kutokana na madai ya kushindwa kutekeleza maelekezo yake katika kusimamia kesi za ukatili mkoani Arusha.
Rc, Makonda amefikia hatua hiyo leo Julai 08, 2024 mara baada ya kupata malalamiko kutoka kwa Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Memuto, Bi. Rose Njilo aliyelalamika kwa Mkuu wa Mkoa kuhusu kutotekelezwa kwa maagizo yake aliyoyatoa wakati wa programu yake ya kusikiliza kero za wananchi iliyofanyika mwishoni mwa mwezi Mei, 2024.
Bi. Rose amemuambia Mkuu wa Mkoa kuwa yupo mtoto anayefahamika kwa jina moja la Witness ambaye alifanyiwa ukatili wa kingono na baadae maagizo kutolewa, lakini kufikia hii leo hakuna hatua yeyote iliyochukuliwa huku binti huyo akipewa vitisho vya kuuwawa suala linalomfanya kutamani kujitoa uhai wake kutokana na vitisho hivyo.
Mhe. Makonda kwenye Mkutano wa wadau wa mashirika na asasi za kiraia zinazoshughulika na maendeleo ya huduma za jamii, ameagiza kufanyika kwa kikao hicho kesho Jumanne Julai 09, 2024 ofisini kwake Jijini Arusha.






0 Comments