Header Ads Widget

PROF NDAKIDEMI AELEZA MIRADI YA MAENDELEO ILIYOTEKELEZWA KATIKA KATA YA OLDMOSHI MASHARIKI KWA KIPINDI CHA MIAKA MINNE.

 


NA WILLIUM PAUL, MOSHI. 



IMEELEZWA kuwa kiasi cha  shilingi bilioni  6,106,516,794.00  zimetumika kwa ajili ya kutekekeza miradi ya maendeleo katika Kata ya Oldmoshi Mashariki katika Jimbo la Moshi vijijini.


Hayo aliyasema Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Profesa Patrick Ndakidemi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika ofisi za Kata ya Oldmoshi Mashariki  uliohudhuriwa na Diwani wa Kata ya Oldmoshi Mashariki Jane Mandara,  Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu, viongozi wa CCM na Serikali kutoka Kata ya Oldmoshi Mashariki na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa MUWSA, Flora Nguma. 



Profesa Ndakidemi alisema kuwa maendeleo makubwa ya miradi ya afya, elimu, barabara, pamoja na maji  yaliyofanyika Oldmoshi Mashariki kwa miaka minne kwa kupitia fedha walizopewa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mkubwa kutoka Mbunge na Diwani wa Kata hiyo, Jane Mandara na viongozi wa Chama na Serikali Wilayani na Mkoani Kilimanjaro pamoja na watendaji wote wa Serikali.


Profesa Ndakidemi amesema kuwa kwa kipindi cha miaka minne serikali imetoa Shilingi bilioni  6,106,516,794.00 kwa miradi ya maendeleo katika kata ya Oldmoshi Mashariki. 



Mbunge aliishukuru sana serikali kwa kuwajengea wananchi wa Oldmoshi Mashariki shule ya Sekondari ya wasichana ya Kidato cha 5 na 6 iliyoigharimu Shilingi Bilioni moja ambapo katika ukaguzi wa mradi huo, Mbunge aliridhishwa na ujenzi wa kiwango cha juu uliofanywa na mafundi wenyeji.


Prof Ndakidemi amewataka wananchi wa Oldmoshi Mashariki waendelee kuiunga mkono Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwenye kata yao na kuwaomba kuepukane na propaganda za aina yeyote ile zinazolenga kuchelewesha maendeleo katika jamii yao. 



Katika mkutano huo, Mbunge Ndakidemi aligawa miche bora ya migomba kwa wananchi. 


Wananchi wengi waliopata fursa ya kuongea katika mkutano huo, walieleza kukerwa na uhaba wa maji katika Kata hiyo. 



Akijibu kero hiyo, mwakilishi wa MUWSA, Flora Nguma alisema kwamba taasisi yake  itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya Maji katika Kata ya Oldmoshi Mashariki.


Aliwaomba wananchi na viongozi wa Vijiji na Kata kutoa ushirikiano ili kufanikisha azma yao badala ya kupinga mipango kabambe ya Serikali ya kuwapatia wananchi huduma ya maji.



Katibu wa CCM wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu amewataka wananchi wa Kata ya Oldmoshi Mashariki kushirikiana na Mbunge na Diwani ili waendelee kunufaika na neema ya miradi kutoka katika serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan. 


Mwisho...

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI