Na Thobias Mwanakatwe,ITIGI
KIONGOZI wa Mbio za.Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Mnzava,amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kujenga kituo cha mkongo wa Taifa katika Halmashuri ya Itigi ambacho kitarahisisha mawasiliano katika mikoa ya Singida,Tabora,Mbeya na Songwe.
Ametoa pongezi hizo jana (Julai 6, 2024) baada ya Mwenge wa Uhuru kutembelea kituo hicho ikiwa ni mwendelezo wa mwenge huo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo iliyotekelezwa katika Halmashuri ya Itigi wilayani Manyoni.
"Kituo hiki kitakuwa na msaada mkubwa katika mkoa ya Singida,Tabora,Mbeya na Songwe katika suala la mawasiliano kwa hiyo niwapongeze TTCL kwa ujenzi wa kituo hiki," amesema Mnzava.
Naye Meneja wa TTCL Mkoa wa Singida, Augustino Mwakyembe alisema kituo hicho kitaongeza ubora na uwezo wa kutoa huduma za mawasiliano na mtandao katika taasisi za kifedha ,Serikali,Mashirika ya Kidini na Matumizi ya kila mwananchi.
Alisema pia kuongeza wigo kwa wakezaji kwa upatikanaji wa mtandao na hasa kutoa nafasi kwa watoa huduma wengine kwa ajili ya huduma ya co location.
Aidha,Mwakyembe aliwaomba wananchi wa Halmashauri ya Itigi kutunza na kulinda kiyuo hicho ambapo aliitikia wito wa mkimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa kupanda miti 50 ndani ya siku tatu.
"Mawasiliano bora yanakuza biashara na huduma mbalimbali Mawasilano bora yamekuwa kivutio cha wawekezaji katika Halmashauri yetu
Mawasiano bora yamechochea usimikaji wa mifumo ya kielektronik na kutuwezesha kukusanya na kudhibiti makusanyo ya mapato," Amesema.
Ameongeza kuwa wanufaika wa mradi huu ni wananchi wakazi wa Itigi, wafanyabiashara, taasisi zote pamoja na Mikoa ya Singida, Mbeya na Tabora na kwamba matarajio ni kuwezesha upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kwa Mkoa wa Singida, Tabora na Mbeya ili kusaidia kukuza uchumi wa jamii pamoja na nchi.
"Sisi wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, kwa heshima kubwa tunamshukuru sana Mhe. Rais kutoa fedha Sh. Bilioni 1.3. kwa upande wa Kituo cha Itigi pekee kwa ajili ya ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano Kata ya Majengo na tunaahidi kuutunza mradi huu ili uendelee kuinufaisha jamii na kwa maendeleo endelevu,"amesema.
Awali Msimamizi wa Kituo cha Mkongo wa Taifa Itigi, Hussein Pungu akisoma taarifa ya mradi amesema mradi wa ujenzi wa Kituo cha Usafirishaji na Usambazaji wa Mawasiliano njiia ya Itigi unaelekea Malongwe hadi Tabora na Kiombo, Rungwa hadi mkoani Mbeya.
Alisema mradi huu kwa mujibu wa mkataba ulianza kutekelezwa Februari 4, 2022 na ulikamilika Machi 1, 2024 ukiwa na jumla ya Kilomita 192 - kilometa 110 (Itigi-Malongwe) na kilomita 82 (Itigi-Kiombo) za mkongo wa mawasiliano kwa upande wa Itigi na ujenzi wa nchi nzima una jumla ya Kilomita 4,442 na vituo wezeshi 111 kikiwepo kituo hiki cha Itigi.
Alisema kituo cha Itigi kilijengwa na mkandarasi mzawa aitwae Mtitima na kwa upande wa ufungaji mitambo umefanywa na Kampuni ya Softnet akishirikiana na Huewei, ikiwa ni nyongeza ya mkataba wa mitambo ya mawasiliano na umeme.
Pungu alisema kiasi cha Sh.milioni 118 zimetumika katika ujenzi wa jengo, uzio, choo na kibanda cha mlinzi na Sh. Bilioni 1.182 na gharama za vifaa vya mawasiliano na mitambo, ikiwa ni fedha kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa kukamilisha kituo cha mkongo wa mawasiliano Itigi.
MWISHO
0 Comments