Header Ads Widget

MSAADA WA MBUNGE NJEZA WAIFUTA MACHOZI FAMILIA, MWANAFUNZI.


NA JOSEA SINKALA, MBEYA.


Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran M. Njeza, amempatia msaada wa fedha shilingi laki sita mtoto Felister Yohana Mwachilinga, ambaye alifaulu kwenda kidato cha tano lakini akashindwa kutokana na familia yake kutokuwa na fedha zaidi ya shilingi laki tano na nusu kumudu gharama za kumpeleka shule binti yao huyo.


Mbunge Njeza ametoa fedha hizo kufuatia mtoto huyo wa kike kutoka kitongoji cha Mshkamano kata ya Nsalala Mbalizi kufaulu kutoka shule ya wasichana Garijembe hivyo familia kuomba msaada kwa wadau ambao walianzisha mchango kupitia kundi la WhatsApp.


Baada ya kupata taarifa za mtoto huyo, Mbunge Njeza amesema kwa mtoto kama huyo mwenye nia ya kusoma ni lazima atiwe moyo ili kufikia ndoto zake hivyo kuendelea kuwaasa wazazi na walezi kuwekeza kwenye elimu maana ndio utajiri wa na urithi wa kweli siku za usoni.


Pamoja na hayo Mbunge huyo amemuahidi mwanafunzi huyo kuwa ataendelea kushirikiana naye katika safari yake ya masomo pamoja na kumpatia fedha hizo (Tsh.600,000/=) kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya shuleni kuhakikisha anatimiza ndoto zake.


Diwani wa kata ya Nsalala Mhe. Ferdinand Mnyota ameshukuru Mbunge pamoja na wote walioguswa na uhitaji wa mtoto huyo kupigania elimu.


Mtoto Felister Yohana Mwachilinga ni mwanafunzi ambaye amehitimu kidato cha nne katika shule ya wasichana Garijembe ambapo amefaulu kwa kupata daraja la kwanza (la point 13) na kuchaguliwa kujiunga katika shule ya upili Lufilyo Tukuyu wilayani Rungwe kwa mchepuo wa PGM hivyo amesaidiwa kutokana na wazazi wake kutokuwa na uchumi mzuri kumudu gharama hizo za kwenda kuanza masomo.


Familia ya binti huyo wamemshukuru Mbunge wa jimbo la Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza kwa msaada wake huo pamoja na watu wengine walioanzisha mchango kumchangia mtoto huyo kupitia kundi la WhatsApp.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI