NA JOSEA SINKALA, MBEYA.
Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza ameendelea na ziara yake jimboni kwake ambapo amefanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Chang'ombe kata ya Mjele akiendelea kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Akiwa katika vijiji vya Chang'ombe na Mjele kwa wakati tofauti, Njeza amekumbana na kero ya barabara ya Mbalizi Chang'ombe hadi Mkwajuni na Makongolosi ambayo imekuwa kero kwa siku za hivi karibuni.
Dotto Gunza ni mkazi wa kijiji cha Chang'ombe, amewataka wahandisi wa barabara kutoka TANROADS mkoa wa Mbeya kurekebisha barabara hiyo kwani kwa hivi karibuni imeharibika zaidi tofauti na hapo awali.
Amesema barabara hiyo imekuwa na vumbi kupita kawaida tofauti na awali ambapo alikuwa wakiweka kifusi kuzuia vumbi lakini upande wa mkoa wa Songwe kwenye barabara hiyo kunapitika vizuri hivyo kuwaomba wataalam hao kurekebisha barabara hiyo kuwa rafiki wakati wakisubiri kuwekewa lami.
Pamoja na kuungana na wananchi wake kuhusu umuhimu wa barabara hiyo, Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Manasse Njeza, amewahakikishia wananchi kuwa itajengwa kwa kiwango cha lami.
Kaimu meneja wa Wakala wa ujenzi wa barabara Tanzania TANROADS mkoa wa Mbeya Mhandisi Mbaza amewahakishia na kuwaondoa hofu wananchi na watumiaji barabara hiyo kuwa itajengwa kwani tayari Serikali imetoa fedha za kuanza kilomita sita kutoka Mbalizi.
Mhandisi Mbaza anasema baadhi ya maeneo yamekuwa korofi ndio chanzo cha kuwepo kwa vumbi kupita kawaida na kuahidi TANROADS kuendelea kufanyia marekebisho barabara hiyo ili kupitika vizuri.
Pamoja na mengineyo Mbunge wa Mbeya vijijini Mhe. Oran Njeza amewaasa wananchi hususani jamii ya kisukuma alioteta nao pembezoni mwa mkutano baada ya mkutanoni wake, kusomesha watoto wao badala ya kuwekeza kwenye ufugaji pekee.
Baada ya mkutano huo katika kijiji cha Chang'ombe, Mbunge Njeza amefanya mkutano katika kijiji cha Mjele na kueleza mambo mbalimbali yaliyotekelezwa katika kata ya Mjele ikiwemo usambazaji umeme hadi vijijini, huduma ya maji na uboreshaji sekta ya elimu.
0 Comments