Na WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa Jimbo la Moshi Vijijini Prof. Patrick Ndakidemi ameendelea na ziara yake jimboni kwa kutembelea Kata ya Kindi na kufanya mkutano wa hadhara katika eneo la Kindi KNCU.
Katika ziara hiyo Mbunge aliongozana na Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Moshi vijijini, Ramadhan Mahanyu, Katibu wa Wazazi wilaya, Andrew Mwandu, Samweli Kirumbuyo (Diwani), viongozi wa CCM na Serikali Kata ya Kindi.
Katika mkutano huo, Mbunge Ndakidemi aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM katika Kata ya Kindi kwa kipindi cha miaka minne tokea aingie madarakani.
Mbunge aliainisha miradi yote ya maendeleo iliyotekelezwa kwenye Kata ya Kindi ambapo takriban jumla ya Shilingi bilioni 3,435,167,923.00 zimetumika katika miradi ya Elimu, Barabara, Afya, Mikopo kwa jamii na Ujenzi wa Ofisi za Kurasimisha Ardhi.
Baadaye wananchi walipata fursa ya kumweleza kero zao ambapo kubwa zilihusisha Ubovu wa Barabara za Ndani, Uchakavu wa madarasa ya baadhi ya shule za msingi zilizopo kwenye Kata na uchakavu wa Zahanati ya Kindi, kukosekana Zahanati katika eneo la Kindi Msasani, Uchakavu wa Mifereji ya Asili na upotevu wa fedha katika SACCOS ya Kindi.
Mbunge alishauriana na diwani na kuchukua kero zote zilizotolewa na aligawa miche bora ya kilimo.
Akizungumza kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya, Katibu wa CCM, Mahanyu alimshukuru Mbunge na Diwani kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwaletea wananchi wa Kindi miradi ya maendeleo.
Aliwashauri Watanzania waendelee kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani anaiongoza Serikali ya awamu ya sita kwa umahiri na weledi mkubwa katika kuhakikisha Taifa na Wananchi kwa ujumla wanasonga mbele kimaendeleo.
Akishukuru, Mwenyekiti wa CCM kata ya Kindi Juma Mwisi alimshukuru mbunge kwa kuwatembelea, na kumwambia kwamba wana Kindi wako naye bega kwa bega kwani yaliyofanyika katika Kata yote ni makubwa na yanaonekana.
Mwisho...
0 Comments