Header Ads Widget

MBIO ZA TANFOAM KUFANYIKA DISEMBA 1 MWAKA HUU ARUSHA

 








Na Pamela Mollel,Arusha

Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Mh,Mrisho Gambo amezindua rasmi mbio za Tanfoam zinazotarajiwa kufanyika Disemba 1,mwaka huu katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Mkoani Arusha

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha,Gambo anasema Marathoni hiyo ni fursa kubwa kwa wakazi wa Arusha kwakuwa mbio hizo zinakwenda kuleta watu wengi zaidi hivyo tukio hilo litachochea uchumi wa Arusha

Anasema kuwa kupitia mbio hizo wajasiriamali mbalimbali watapata fursa ya kuuza bidhaa zao kwa kuwa ndani ya uwanja huo kutakuwepo na mabanda ya wajasiriamali 

“Hii ni fursa kubwa Tanfoam wametuleta Arusha,kina mama pamoja na vijana wajasiriamali watapata fursa ya kuuza bidhaa zao lakini pia hoteli zetu zitapata wageni “anasema Gambo

Pia aliongeza kuwa mbio hizo zinakwenda kuchochea utalii wa ndani kutokana na wageni mbalimbali waliofika kwaajili ya mbio hizo kwenda kutembelea Mbuga za wanyama kama vile Arusha National park,Tarangire,Ngorongoro na maeneo mengine 

Aidha aliwataka wadau mbalimbali wakiwemo watu wa hifadhi kuwaunga mkono Tanfoam kwa kuja na fursa hiyo ambayo itasaidia kuboresha afya katika jamii

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha mauzo na masoko Tanfoam Ltd,Glorious Temu anasema lengo kuu la mbio hizo ni kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi na kulala vizuri ili kuboresha afya na utendaji

“Tumejikita zaidi kusambaza ujumbe muhimu wa afya ya kimwili na akili kupitia michezo ambapo sehemu ya michango ya ununuzi wa mfuko wa mbio za Tanfoam itarudishwa kwa jamii,ambapo mfuko wa mbio ni shilingi elfu thelasini na tano (35,000,)anasema Glorious

Alitaja mbio hizo kuwa ni za kilometa 21,10 na 5 huku zawadi ya mshindi wa kwanza akijinyakulia kitita cha shilingi milioni tano,mshindi wa pili shilingi milioni mbili na mshindi wa tatu shilingi milioni moja pamoja na bidhaa za Tanfoam

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI