Na Fadhili Abdallah,Kigoma
MBUNGE wa jimbo la Kigoma Kaskazini Asa Makanika ameitaka serikali kupitia wizara ya nishati kuwawajibisha wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini (REA) kwa kushindwa kutimiza majukumu yao na kuwachonganisha wananchi na viongozi wao.
Makanika alisema hayo akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Mkongoro halmashauri ya wilaya Kigoma akitoa kauli ikiwa majibu ya malalamiko ya wananchi wa Kijiji hicho wakiwalalamikia wakandarasi hao kushindwa kuleta umeme kwenye maeno yao kwa Zaidi ya miaka minne sasa.
Kufuatia hali hiyo Mbunge huyo wa jimbo la Kigoma Kaskazini alisema kuwa hali hiyo haitakubalika na hatakubali kuona wakandarasi wakitoa ahadi za uongo huku miradi ya kuleta umeme kwenye vitongoji haikamiliki hivyo alisema kuwa anatarajia kukutana na Waziri wa nishati kueleza kilio hicho na wakandarasi wasiotekeleza mikataba yao wawajibishwe.
Makanika alisema kuwa serikali ya awamu ya sita imeuachagua mkoa Kigoma kuwa kitovu cha biashara kwa nchi za maziwa makuu na mkoa wa kimkakati kwa ajili ya uchumi wa nchi na biashara hivyo kupelekwa umeme vijijini na kwenye vitongoji kuna umuhimu mkubwa katika kutekeleza amza hiyo ya serikali.
Awali wananchi wa Kijiji hicho akiwemo , Richard Vugamake na Kyumba Hatibu kutoka kitongoji cha CCM Centre walisema kuwa wamekuwa wakipewa ahadi za uongo na wakandarasi hao kwa Zaidi ya miaka minne sasa hali ambayo inawaondolea Imani ya kutekelezwa kwa miradi ya kuletwa umeme kwenye maeneo yao huku wakiwa wametandaza mtandao wa umeme kwenye nyumba zao na Kijiji kufanyiwa savei lakini umeme haijafika kwenye kitongoji chao hadi sasa.
Akitoa maelezo kuhusu utekelezaji wa miradi ya REA kwenye wilaya ya Kigoma Mhandisi wa TANESCO anayesimamia miradi ya umeme vijijini katika wilaya hiyo, Joseph Kanje alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya utekelezaji wa miradi hiyo kutokana na kuchelewa kupatika kwa fedha lakini kwa sasa miradi kwenye wilaya hiyo itaanza mwishoni mwa mwezi huu.
0 Comments