Thobias Mwanakatwe, Matukio Daima Media- ITIGI
HALMASHAURI za Wilaya nchini zimeagizwa kuweka utaratibu wa kununua dawa ya kupulizia kwa ajili ya kuua mazalia ya mbu katika robo ya kwanza au ya pili ya kila mwaka wa fedha ili kutokomeza ugonjwa wa malaria kama ilivyoagizwa na rais Dk.Samia SuluhuHm Hassan.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava, ametoa agizo hilo leo (Julai 6, 2024) baada ya kutembelea ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Itigi mkoani Singida na kupewa taarifa ya programu ya malaria katika Halmashauri ya Itigi.
"Kuna mtindo kwenye halmashauri suala hili linapelekwa mwishoni kabisa kwenye mwaka wa fedha unasikia hii tunatekelezaga robo ya mwisho,sikatai labda kutokana na jiographia lakini kwanini dawa ikinunuliwa robo ya kwanza au ya pili je ita-expire mbona dawa nyingine zinanunuliwa," alihoji.
Mnzava ametoa agizo hilo baada kuelezwa kuwa katika kipindi cha mwaka 2021, 2022 na 2023 dawa hizo hazijapulizwa katika halmashauri hiyo na hivyo kuhoji je wananchi waliogua ugonjwa wa malaria katika kipindi hicho wataweza kufidiwa.
"Mimi naogopa kama kiongozi wa mkuu wa nchi anaelekeza jambo hakafu kuna watu hawataki kutekeleza,je hawa waliopata Malaria katika kipindi ambacho dawa haijapulizwa watafidiwa," alisema.
Mnzava amesema hapa suala sio la bajeti ambapo zinahitajika Sh.milioni moja tu kununua dawa hizo wakati uwezo wa halmashuri kukusanya mapato yake ya ndani ni zaidi ya Sh.bilioni moja.
"Jana niliuliza wenzeni wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni hii halmashauri ipo bize na nini kama haipo bize kutekeleza maelekezo ya viongozi, na hapa suala sio DC (Mkuu wa Wilaya) au Mkurugenzi bali ni wataalam ambao wanajua uhalisia wa jambo lenyewe lakini hawataki kutekeleza," amesema Mnzava.
Awali Mratibu wa Malaria Halmashauri ya Itigi, Monica Paul, amesema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Disemba 2023 vyandarua 56,678 viligawiwa kwa wazee na wajawazito na watoto waliopata chanjo ya surua ya kwanza walikuwa 11,573.
Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Itigi imetenga Sh.milioni 1.492 katika kipindi cha mwaka 2023/2024 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na upuliziaji wa viuadudu ambazo Sh.600,000 zimeshalipwa kwa ajili ya kununua viuadudi lita 46.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Manyoni,Kemirembe Lwota, amesema atahakikisha anasimamia suala la ununuzi wa dawa ya viuadudu katika halmashuri zilizopo katika wilaya hiyo Itigi na Manyoni ili kutimiza azma ya serikali ya kupunguza ugonjwa wa malaria.
MWISHO
0 Comments