Na Fatma Ally, Matukio DaimaApp, Dar
Aliyekuwa mgombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) Doyo Hassan Doyo amesema uchaguzi uliofanyika Juni 29 Katika Hotel ya Ramada Ilala jijini Dar es Salaam ni batili kwani umekiuka sheria na kutozingatia katiba ya chama.
Aidha, yeye pamoja wajumbe 70 wamekata rufaa ya kupinga matokeo ya uchaguzi kwa kutozingatia Katiba na kanuni za Chama, kwani uchaguzi huo umesimamiwa na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake jambo ambalo sio halali kwani aliyepaswa kusimamia uchaguzi huo ni mwenyekiti wa mpito.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Doyo amesema kuwa uchaguzi huo ulikuwa batili hawautambui na urudiwe tena na usimamiwe na Msajili wa vyama vya siasa.
Ameongeza kuwa tayari wamepeleka rufaa ya kupinga matokeo hayo kutokana na kuvunjwa vifungu vya Katiba ya chama hicho ikiwemo mkutano kuongozwa na Mwenyekiti anaemaliza muda wake badala ya Mwenyekiti wa muda anaeteuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha Katiba ya chama.
"Mwenyekiti wa muda kwa mujibu wa kifungu hiki anatakiwa kusimamia uchaguzi wa nafasi ya uchaguzi hivyo kitendo Cha Mwenyekiti anaemaliza muda wake Hamad Rashid kusimamia mkutano Mkuu wote Hadi chaguzi za makamu Mwenyekiti Kwa upande wa Bara na Zanzibar amevunja kanuni za Chama hivyo uchaguzi uliofanyika ni batili "amesema Doyo.
Aidha ameongeza kuwa taratibu za kupiga kura pia hazikuzingatiwa kwani wajumbe walikuwa wamezidi idadi inayotakiwa ambapo rejesta inayopelekwa kwa Msajili wa vyama vya siasa haikutumika hivyo kuongeza idadi ya kura za wajumbe halali 192 na kuwepo kwa kura 200.
Sambamba na hayo amesema viongozi wapya wengi waliochaguliwa ni aliwachagua mwenyewe mwenyekiti anaemaliza muda wake, Hamad Rashid, hivyo inadhihirisha kuwa kusema kuwa anamaliza muda wake ila upande wa pili anakitaka Chama Kwa mgongo wa nyuma.
Hata hivyo Doyo amewashukuru wapiga kura 70 waliomwamini na kumpigia kura kati ya wajumbe halali 192 ambapo kwenye sanduku zilikutwa kura 200 ambapo kura hizo ni sawa na Kanda 7 kati ya 10.
Amesema hawajatukana wala kumsakama mtu wameamua kukata rufaa kwa kufata misingi ya kikatiba na wanategemea kujibiwa kwa kufata misingi ya kikatiba na kanuni na ikishindikana wataenda kutafuta haki mahakamani.
0 Comments