Header Ads Widget

CHADEMA VWAWA YAPANIA KUIONDOA CCM UCHAGUZI UJAO.



NA JOSEA SINKALA, SONGWE.


Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Vwawa mkoani Songwe Mchungaji Amoni Mwashitete amewataka wananchi kuhakikisha wanajiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili kuchagua viongozi bora kwa maendeleo yao akidai CCM haina kibali cha kuongoza.


Mchungaji Mwashitete amesema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Ichenjezwa Vwawa mkoani Songwe.


Amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi imeshindwa kuwaletea wananchi maendeleo hivyo kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu lazima wananchi waungane kuichagua CHADEMA akihusisha na hali halisi ya maisha ya wananchi kuwa yamekuwa magumu na maendeleo ya kusuasua katika nyanja mbalimbali.


Seleman Mgalla ni katibu mwenezi wa CHADEMA jimbo la Vwawa, anasema CHADEMA ina hoja nyingi za kuendelea kuwaelimisha wananchi kuwa CCM imeshindwa kuwaletea maendeleo na kwenye chaguzi zijazo lazima waikatae.


Mwenezi huyo anasema katika mji wa Vwawa hali ya barabara bado ni mbaya, huduma ya maji haipatikani katika maeneo yote, utitiri wa kodi na ushuru kwenye biashara na mazao ya wakulima na nyinginezo.


Viongozi, wanachama na wafuasi wa Chama hicho wanasema wamejipanga ipasavyo kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI