CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Singida kimelalamikia ĥujuma za kukamatwa ovyo kwa viongozi wanaoendesha zoezi la usajili wa wanachama kidigitali unaoendelea kwenye majimbo saba ya mkoa huu.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida,Jackson Jingu, akizungumza leo (Julai 18,2024) na waandishi wa habari amesema chama hicho kina usajili wa kufanya siasa kama vyama vingine kwa uhuru na haki hivyo hujuma wanazofanyiwa katika zoezi la usajili wanachama halina afya kisiasa.
"Tunatoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na tunapotoa taarifa hizi wawe wanasimamia misingi na utawala bora kwa kuwasihi wenzetu wa chama tawala wasifanye mambo haya ambayo yanaleta taharuki na tunamuomba RPC achukue hatua," alisema Jingu.
Kuhusu kauli iliyotolewa na Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ya ushindi nje ya box la kura, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida alisema kauli yake haiwatishi na badala yake imewasaidia kujua ukweli na hivyo kujipanga katika chaguzi zijazo.
0 Comments