NA JOSEA SINKALA MBEYA.
Vuguvugu la upatikanaji wa Katiba mpya nchini Tanzania linaendelea ambapo wananchi wanaitaka Serikali kuendelea na tume ya Jaji Joseph Warioba ili Tanzania kupata Katiba mpyana bora itakayoendana na wakati wa sasa.
Wananchi kutoka makundi mbalimbali katika jamii Mkoani Mbeya wametoa maoni hayo kwenye kikao cha mjadala wa wazi juu ya mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.
Ezekiel Mwampaka ni Wakili wa kujitegemea kutoka kundi la wanasheria, anasema ni muhimu Tanzania kupata katiba mpya.
"Asante wawezeshaji kwa mawasilisho yenu, kwanza niseme TLS (Chama cha mawakili wa Tanganyika) tumechelewa sana na mimi niseme tu ni muumini wa Serikali tatu, baadhi ya watu wanajiuliza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitakuwa na fedha basi mjue tu hayo ni mawazo mfu kwasababu mabillion tu yanayopotea kwa mujibu wa CAG yana nafasi kubwa kuendesha Serikali ya Jamhuri", Amesema Wakili Mwampaka.
Kwa upande wake Agatha Daud Kaleke ambaye ni Mwananchi Mkoani Mbeya na Mjumbe wa Serikali ya mtaa mmoja wapo mkoani humo amesema malumbano hayapaswi kushuhudiwa miongoni mwa wananchi badala yake waungane kudai katiba mpya bila ubaguzi wowote ili kufikia maendeleo endelevu.
Naye Mhandisi maneno Sanga ameshauri wasomi wakiwemo mawakili pamoja na kuzingatia maoni ya wananchi kupitia makundi mbalimbali pia watoke na hoja ya pamoja ili kufanikiwa kuwa na katiba iliyoboreshwa kuanzia kwenye katiba ya sasa ya mwaka 1977.
Alipopata nafasi ya kuchangia kwenye mjadala huo wa wazi uliowakutanisha watu mbalimbali, Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa Joseph Mbilinyi (Sugu), amesema katiba mpya ni hitaji la wananchi la muda mrefu pamoja na tume huru ya uchaguzi.
Sugu amesema wanaogoma kupatikana kwa katiba mpya ni wanufaika wa katiba ya sasa kutaka kuendelea kusalia madarakani bila uwajibikaji mzuri wa viongozi kwa wananchi mambo ambayo anasema Serikali ya CHADEMA haitavumilia.
Akizungumza kwenye mjadala huo, mmoja wa wawezeshaji/watoa mada, Mjumbe wa bodi ya jukwaa la katiba nchini Tanzania Deus Kibamba ameainisha madhaifu mbalimbali ya katiba ya sasa (ya 1977) hivyo kuonyesha umuhimu wa wa-Tanzania kuungana kudai katiba mpya kuanzia kwenye maoni ya Jaji Joseph Sinde Warioba.
"Niwaambie mmeiona hii ni rasimu ya Jaji Warioba natamani kuibusu, kwenye nchi hii jaji Joseph Warioba amevunja rekodi (historia) ya kufanya kazi nzuri sana ya kukusanya maoni haya, wapo watu wanaosema aliwahoji wangapi, kiukweli kwenye jambo kama hili huwezi kuwafikia watu wote lakini kwa utafiti wangu mimi binafsi watu waliotoa maoni kwa njia tatu za kumfikia jaji Warioba, kutuma maoni au kwa namna nyingine yoyote wamefikia nusu ya wa-Tanzania wote hapa nchini (zaidi ya watu million 30)", ameeleza Kibamba.
Mbobezi huyo wa masuala ya sayansi ya siasa amesema ni wakati muafaka sasa Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuruhusu mchakato wa Katiba mpya kupitia rasimu ya Jaji Joseph Warioba kwakuwa Katiba ni matakwa na mali ya wananchi badala ya katiba ya sasa ambayo imefanyiwa marekebisho mara kadhaa lakini bado haiendani na wakati huku ikiwa na mamlaka makubwa kwa Rais wa nchi badala ya wananchi.
Kwa upande wake Rais mstaafu wa Chama cha wanasheria wa Tanganyika (TLS) Wakili Francis Stolla, amesema kwa mujibu wa katiba ya sasa Rais wa Tanzania anaweza kushtakiwa kwa kosa la madai pekee lakini kwa kesi ya jinai hatakiwi kushtakiwa kwakuwa amewekewa kinga na katiba miongoni mwa mambo ambayo hayana budi kuangaliwa kwenye katiba mpya.
Chama cha wanasheria wa Tanganyika TLS hapa nchini kinaendelea kuendesha mijadala ya wazi ili kuendelea kuwajenga, kuwasikiliza na kupokea maoni ya wananchi kuhusu namna bora kutoka kwenye mkwamo wa Katiba ya mwaka 1977 inayotumika sasa ili kupata Katiba mpya ambayo inatajwa kuwa hitaji la wananchi katika uendeshaji wa Taifa lao kwa maendeleo endelevu.
0 Comments