Na Shemsa Mussa. Kagera
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameukumbuka Mkoa Kagera kupitia program yake mpya ijulikanayo kama Mama Samia Mentorship baada ya kutuma timu ya madaktari bingwa wa huduma za Mkoba za kibingwa na ubingwa bobezi wapatao 40 kutoka hapa Nchini ikiwa lengo ni kusogeza huduma za Afya karibu na Wananchi ikiwa ni pamoja na kuokoa gharama na muda wa kufuata huduma hizo nje ya Mkoa huo.
Akizungumza katika uzinduzi wa Huduma hizo uliofanyika Juni 17, 2024 katika Hospitali ya Manispaa ya Bukoba(Nshambya) Grace Aminiel Mariki ambaye ni Afisa idara ya Afya ya uzazi Mama na mtoto alisema lengo la ujio huo katika Mkoa wa Kagera ni kufikisha huduma ya Mama Samia Mentorship kwa Wananchi wa Kagera katika Halmashauri 8 za Mkoa huo ambapo wanategemea kuwafikia Wananchi wote katika maeneo yao lengo kubwa likiwa ni kuhakikisha huduma za matibabu zinawafikia Wananchi kwa gharama nafuu katika maeneo badala ya kusafiri umbali mrefu.
Bi Grace, amewataja madaktari hao waliopokelewa kuwa ni pamoja na Madaktari bingwa wa Watoto, Magonjwa ya Wanawake na ukunga, upasuaji na ubobezi wa mfumo wa mkojo, Usingizi na ganzi, Magonjwa ya ndani na Magonjwa mengineyo huku akisema wanatarajia kuwafikia Wananchi wengi kwani huduma hiyo itatolewa kwa wiki nzima katika Hospitali zote za Wilaya ndani ya Mkoa huo huku akiwaomba Wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupokea huduma hizo.
"Mradi wa Mama Samia Mentorship unatekelezwa katika Mikoa 26 Nchini tayari tumefikia Mikoa 23 Halmashauri 139 Kati ya Halmashauri 184 hapa Nchini sasa ni zamu ya Kanda ya ziwa na tayari tumepata mafanikio makubwa kwani tumewafikia Wananchi zaidi ya elfu 50 lakini pia zaidi ya Wananchi elfu 3 wamepata huduma za upasuaji wa kibingwa bobezi kutoka kwa madaktari bingwa waliopelekwa katika Hospitali za Halmashauri"alisema Grace.
Naye mgeni rasmi katika uzinduzi wa Huduma za Mkoba za kibingwa na ubingwa bobezi Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Siima kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera alimshukuru Rais Samia kwa jitihada zake za kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha anaboresha huduma za Afya kwa Wananchi na Watanzania kwa ujumla huku akiwataka Wananchi wenye matatizo kujitokeza kwa wingi kupata huduma hiyo.
"Rais Samia amesaidia sana kuhakikisha Afya za Watanzania zinaimarika kila siku sasa kazi iliyobaki ni kujitokeza kwa wingi" alisema Erasto.
Aidha naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Jacob Simon Nkwera alimpongeza Rais Samia kwa kutoa huduma hiyo huku akiahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kama ilivyokusudiwa.
Hata hivyo kwa upande wao Wananchi wa kata ya Nshambya Manispaa ya Bukoba waliofika kwa ajili ya kupata matibabu akiwemo Bi Happynes Justace na Richard Rugaika wamemshukuru Rais Samia kwa kuwatuma Madaktari hao kwani kwao imekuwa ni faraja na kwa wengine baada ya kuwaondolea gharama ambazo wangetumia kwenda kutibiwa mbali na kwa gharama kubwa.
0 Comments