Header Ads Widget

NKOSWE HATIANI KWA KUKUTWA NA MENO YA TEMBO NA KIBOKO

Na Moses Ng'wat, Songwe.

JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe limemkamata Boniface Nkoswe (34) Mkazi wa Kijiji cha Nambala, Kata ya Mlowo, Wilayani Mbozi kwa tuhuma za kukutwa na nyara za serikali ambazo ni vipande 13 vya meno ya Tembo, pamoja na jino moja  la Kiboko.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agostino Senga, amewaambia waandishi wa habari leo Juni 18, 2024 kuwa mtuhumiwa huyo, alikamatwa  Juni 15, 2024, majira ya saa 12:00 Alfajiri katika moja ya  nyumba za kulala wageni (jina limehifadhiwa) iloyopo katika eneo la Selewa kata ya Mlowo, Wilayani Mbozi.


Kamanda Senga amesema mtuhumiwa Nkoswe alikamatwa kwa ushirikiano kati ya jeshi la polisi na askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) baada ya kupokea taarifa fiche kutoka kwa wasamalia wema.


Amesema baada ya kupekuliwa mtuhumiwa huyo alikutwa na vipande 13 vya meno ya Tembo, pamoja na jino moja la kiboko ambavyo thamani yake bado haijafahamika hadi sasa vikiwa vimehifadhiwa katika mfuko wa sandarusi.


" Tulifanikiwa kumkamata mtuhumiwa kwa kushirikiana na wenzetu wa TANAPA akiwa na nyara hizo za serikali katika moja ya nyumba za kulala wageni baada ya kupata taarifa za siri kutoka kwa raia wema" amesema Kamanda Senga.


Kamanda Senga amesema mtuhumiwa bado anaendelea kushikiliwa na jeshi la Polisi kwa hatua za  upelelezi zaidi na atafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi huo kukamilika.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI